Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mheshimiwa Solomoni Itunda, akitoa hotuba ya ufunguzi wa kongamano la TAWEN. Akiwa amesimama jukwaani mbele ya washiriki, anasisitiza umuhimu wa uwezeshaji wa wanawake na vijana katika maendeleo ya taifa.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mheshimiwa Solomoni Itunda, akikagua vifaa vya nishati safi vilivyowekwa kwa ajili ya maonesho, ikiwemo mitungi ya gesi, majiko ya umeme (induction cookers) na vipeperushi vya elimu ya matumizi salama. Mh. Itunda alionekana akizungumza na mmoja wa maafisa wa TAWEN huku akionesha shauku na kupongeza juhudi za taasisi hiyo katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, hatua inayolenga kuboresha afya na kukuza uchumi wa wanawake mkoani Mbeya.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mheshimiwa Solomoni Itunda, akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Kongamano la TAWEN
Mbeya, Tanzania 24 Septemba 2025
Mtandao wa Uwezeshaji Wanawake Tanzania (TAWEN) umeendelea kuonesha dhamira yake ya dhati ya kuwawezesha wanawake na vijana kupitia kongamano kubwa lililofanyika jijini Mbeya, ambapo elimu na fursa mbalimbali ziliwasilishwa kwa washiriki kutoka sehemu tofauti za mkoa huo.
Kongamano hilo lilifunguliwa rasmi na Mheshimiwa Solomoni Itunda, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Beno Malisa. Katika hotuba yake, Mh. Itunda alitoa pongezi kubwa kwa TAWEN kwa mchango wao katika kuinua wanawake na vijana, akisisitiza kuwa uwezeshaji wa makundi haya ni kichocheo kikuu cha maendeleo ya taifa.
“TAWEN siyo tu kuwawezesha wanawake na vijana, bali ni taasisi inayogusa maisha ya watu kwa vitendo. Kupitia miradi ya nishati safi na elimu ya ujasiriamali, wamekuwa sehemu muhimu ya mabadiliko tunayoyahitaji. Kama serikali, tunaunga mkono juhudi hizi kwa dhati,” alisema Mh. Itunda.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa taasisi kama TAWEN kuendelea kushirikiana na halmashauri za mikoa na serikali kwa ujumla, ili kuhakikisha kwamba fursa zinazopatikana haziishii mijini tu bali zinamfikia kila mwananchi hadi vijijini.
Hata hivyo, katika ushiriki huo, Mkurugenzi wa TAWEN Tanzania, Bi. Florence Masunga, aliwakilishwa na Bw. Idrissa Sambeli, ambaye aliwasilisha ujumbe rasmi wa uongozi wa TAWEN na kuelezea mafanikio na dira ya mtandao huo kwa miaka ijayo.
Katika kongamano hilo, viongozi wa TAWEN walitangaza kuwa hadi sasa mtandao huo umefanikiwa kufungua matawi 12 nchini, yakiwemo maeneo kama Dar es Salaam, Songwe, Arusha, Iringa, Dodoma, Mbeya, Morogoro, Tanga, Katavi, Mwanza, Pwani, na Zanzibar ambapo Zanzibar imesajiliwa kwa kufuata kanuni za visiwani humo.
Kauli mbiu ya TAWEN kwa wanawake ni “Wakati wa Mwanamke ni Sasa – Inuka!” na kwa vijana ni “Naifikiaje Ndoto Yangu?” Kauli hizi zimekuwa dira ya mabadiliko katika kuhakikisha wanawake na vijana wanatambua haki zao, nafasi zao, na kuchukua hatua madhubuti katika maendeleo ya jamii.
Katika sekta ya nishati safi ya kupikia, TAWEN imefanikiwa kugawa mitungi 750 ya gesi kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali pamoja na kukopesha majiko ya umeme (induction cookers) kwa zaidi ya wanawake 2,000. Hii ni sehemu ya kuunga mkono mpango wa kitaifa wa kuhakikisha wanawake hawabebi tena kuni kichwani ifikapo mwaka 2034, na taifa linafikia matumizi ya nishati safi kwa asilimia 80.
Kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali kama SIDO, BRELA, TBS, pamoja na wadau wa fedha na nishati, TAWEN imewezesha elimu ya ujasiriamali na usajili wa biashara kufikishwa kwa wanawake wa Kigamboni, Ubungo na maeneo mengine. Washiriki wa kongamano la Mbeya walipewa nafasi ya kujifunza, kuuliza maswali na kupata fursa za moja kwa moja.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo aliwahimiza wananchi wa Mbeya kuchangamkia fursa hizi na kuhakikisha elimu na msaada uliopatikana unawafikia wanawake na vijana wengi zaidi. Aliwahimiza pia kujiunga na TAWEN ili kufaidika na mitandao ya mafunzo, mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri, pamoja na elimu ya matumizi sahihi ya nishati safi na ujasiriamali.
Kongamano hilo limeelezwa kuwa chachu ya mabadiliko, mshikamano na mwamko wa maendeleo. Wananchi wa Mbeya wamehimizwa kuwa mabalozi wa elimu, fursa na mabadiliko chanya kupitia mtandao wa TAWEN.
"Ukiona mbali, nenda na wenzako. Wakati wa mwanamke ni sasa, tuamke kwa pamoja."
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464