` WAKULIMA WAPEWA ELIMU KUHUSU MBEGU ZINAZOSTAHIMILI MABADILIKO YA TABIANCHI

WAKULIMA WAPEWA ELIMU KUHUSU MBEGU ZINAZOSTAHIMILI MABADILIKO YA TABIANCHI

    

Ikiwa ni sehemu ya Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, wakulima na wadau wa kilimo wametakiwa kutopitiliza bila kutembelea mabanda ya Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

Katika mabanda haya, wakulima wanapata fursa ya kujionea mbegu mpya za mazao zilizozinduliwa mwaka huu ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Miongoni mwa mbegu mpya zinazopatikana ni Maharage: TARI BEAN 6, 7, 8, 9, 10 na 11, Choroko: TARI G-Gram 1, 2, 3 na 4, Mbegu za mbogamboga

Zote zimeboreshwa ili kuongeza tija, kustahimili ukame, na kuwa na virutubisho vinavyohitajika kwa lishe bora.

Mtaalam na mtafiti wa magonjwa ya mimea kutoka TFSRP, Bi. Edith Kadege, ameeleza kuwa mbegu hizo ni matokeo ya utafiti wa kina ili kutoa suluhisho kwa wakulima.

“Tumekuja na mbegu mbadala wa maharage pendwa aina ya Lyamungo 90. Sasa kuna TARI BEAN 7 ambayo haishambuliwi na magonjwa ya chule. Pia TARI BEAN 6 ni mbadala wa Jeska na ina virutubisho vya zinki na chuma kwa ajili ya lishe, huku ikikomaa kwa muda mfupi,” amesema Bi. Kadege.

Kwa upande wa choroko, mbegu mpya aina ya TARI G-Gram 1–4 nazo zinakomaa kwa muda mfupi na zina virutubisho muhimu vya zinki na chuma, vinavyosaidia lishe ya mwanadamu.

Afisa Mazingira Mwandamizi kutoka TFSRP, Bi. Tulizo Malavanu, amesema baada ya TARI kugundua mbegu hizo, Wakala wa Taifa wa Mbegu (ASA) huzalisha kwa wingi na kuhakikisha upatikanaji wake kwa wakulima.

Hadi sasa, ASA imezalisha zaidi ya tani 12,000 za mbegu zilizothibitishwa na TOSCI, hatua inayowapa wakulima uhakika wa upatikanaji wa mbegu bora na zenye tija.

Wakulima wote kutoka kanda zote nchini wanakaribishwa kutembelea mabanda ya TFSRP na TARI katika viwanja vya Nanenane Nzuguni kujifunza teknolojia mpya za kilimo.

Kwa kujifunza na kutumia mbegu hizi, wakulima watapata suluhisho la changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza kipato kupitia kilimo chenye tija.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464