MWENGE WA UHURU WAMULIKA MIRADI YA MAENDELEO KWA KISHINDO WILAYANI SHINYANGA
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MWENGE wa Uhuru umekimbizwa wilayani Shinyanga,na kumulika miradi 8 ya maendeleo yenye thamani ya sh.bilioni 2.8.
Umekimbizwa leo Agosti 6,2025 na kuongozwa na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025 Ismail Ali Ussi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi kwenye miradi hiyo,ameeleza kufurahishwa na utekelezaji wake, akiipongeza wilaya hiyo kwa kusimamia kwa ufanisi miradi yenye tija kwa jamii.
"Miradi hii ya maendeleo inagusa maisha ya wananchi,na nimeikagua na kupitia nyaraka zake haina ubabaishaji na imetekelezwa kwa kiwango bora kabisa, fedha za Rais Samia Suluhu Hassan mmezitendea haki," amesema Ussi.
Amewataka pia wananchi waitunze miundombinu ya miradi hiyo na kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake, ili idumu kwa muda mrefu kuwahudumia.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, awali akizungumza mara baada ya kuupokea Mwenge huo kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda,amesema ukiwa wilayani humo utakimbizwa umbali wa Kilomita 175 na kumulika miradi 8 ya maendeleo yenye thamani ya sh.bilioni 2.8.
Aidha,miradi iliyo mulikwa na Mwenge wa Uhuru wilayani Shinyanga ni ujenzi wa nyumba ya Afisa Ugani Kata ya Didia,Mradi wa Nishati Safi ya kupikia Shule ya Ola,uzinduzi wa Klabu ya wapinga Rushwa shule ya Sekondari Ilola,Mradi wa uwezeshaji Vijana kiuchumi Ihalo,na Mradi wa Maji Kijiji cha Buzinza.
Miradi mingine ni Uwekaji jiwe la Msingi Kituo cha Afya Lyabukande, Ujenzi wa Machinjio ya kisasa Solwa na uzinduzi wa shule ya Sekondari Amali iliyopo Mwambasha.
Mwenge huo kesho utakimbizwa katika Manispaa ya Shinyanga,ukiwa na kauli mbiu isemayo Jitokeze kushiriki uchaguzi wa mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.