Na Mapuli Kitina Misalaba
Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Ngokolo, Victor Mkwizu, amerejesha rasmi fomu yake ya kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuwania tena nafasi ya udiwani wa kata hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.
Mkwizu ambaye amehitimisha kipindi chake cha uongozi wa miaka mitano, amesema ameamua kurejea tena kwa nia ya kuendeleza misingi ya maendeleo aliyoweka pamoja na wananchi wa Ngokolo katika kipindi kilichopita.
“Nimerudi kwa sababu bado nina ndoto ya kuiona Ngokolo ikisonga mbele zaidi. Tumefanikisha mambo mengi, lakini bado kuna mengi ya kufanya. Naamini kwa ushirikiano na wananchi, tunaweza,” amesema Mkwizu mara baada ya kurejesha fomu.