` CP HAMDUNI AMEZITAKA NGO KULINDA MASLAHI YA NCHI:MKUTANO MKUU WA MWAKA WA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI SHINYANGA

CP HAMDUNI AMEZITAKA NGO KULINDA MASLAHI YA NCHI:MKUTANO MKUU WA MWAKA WA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI SHINYANGA

CP HAMDUNI AMEZITAKA NGO KULINDA MASLAHI YA NCHI:MKUTANO MKUU WA MWAKA WA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI SHINYANGA

Na Maro Maduhu,SHINYANGA

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni, ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) mkoani humo, kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, na mwongozo wa uratibu na usimamizi wa mashirika hayo, huku wakilinda maslahi ya taifa na kuheshimu mila na desturi za Mtanzania.
Amebainisha hayo leo Julai 30,2025 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita,kwenye Mkutano wa Mwaka wa Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani humo, wenye kauli mbiu isemayo,Tathimini ya miaka mitano ya mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya Taifa,Mafanikio, Changamoto na Fursa.

Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali katika kusaidia jamii kupitia sekta mbalimbali, lakini akasisitiza umuhimu wa kuyatekeleza majukumu yao kwa uwazi, uadilifu, na utii wa sheria, bila kuruhusu kutumika kinyume na maslahi ya nchi.
“Serikali inatambua na kuthamini mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika kusaidia jamii, hivyo nawaomba katika utekelezaji wa majukumu yenu lindeni Maslahi ya nchi pamoja na kuheshimu mila na desturi za Mtanzania,”amesema CP Hamduni.

Ametaja michango ya Mashirika hayo kuwa ni uboreshaji wa huduma za Afya, uwezeshaji vikundi vya Vijana hasa akina Mama wadogo na wasichana Balehe kwa kuwapatia mafunzo ya ufundi katika fani mbalimbali,kuwezesha Mkoa kuandaa mpango mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2025/2030.
Michango mingine ni uboreshaji wa huduma za wahanga wa ukatili wa kijinsia kwa kufanikiwa kujenga vituo Jumuishi vya kutolea huduma katika Hospitali ya wilaya ya Kishapu na Msalala, pamoja na kuanzishwa madawati katika maeneo ya umma ikiwamo stend kuu za mabasi na masoko.

Aidha,ameyataka pia mashirika hayo, kuhakikisha wanawasilisha vibali vya utekelezaji wa miradi katika Mamlaka husika kipindi wanapopata miradi mipya, kuwasilisha taarifa za robo mwaka na mwaka ili kuwezesha zoezi la ufuatiliaji na tathimini,kuzingatia misingi ya uwajibikaji wa fedha za miradi,na kuzingatia vipaumbele vya serikali katika mipango yao.
“Nanatambua changamoto iliyowakumba baadhi ya mashirika kwa kusitishiwa ghafla ufadhili kutoka Marekani USAID ,hivyo nitumie fursa hii kuwapongeza kwa utulivu ambao mmeuonyesha katika kipindi hiki kigumu na kuendelea kutoa huduma katika jamii kwa moyo wa kujitolea,”amesema CP Hamduni.

Katika hatua nyingine ameyataka mashirika ambayo yamepata idhini ya kutoa elimu ya mpiga kura kwamba watoe elimu hiyo kwa umakini na kwa kuzingatia uzalendo.
Naye Afisa Maendeleo wa Mkoa wa Shinyanga Bestina Gunje.amesema mkoa huo una mashirika 206 na kwamba Mkoa huo wamekuwa wakishirikiana nayo kwa ukaribu katika kutekeleza Afua mbalimbali zinazogusa jamii hasa katika Sekta ya Maji,Afya,Elimu,Kilimo,Ufugaji,kupinga ukatili wa kijinsia,na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Aidha,ametaja changamoto ambazo hukabiliana na mashirika hayo, kuwa ni baadhi kutekeleza miradi bila kutoa taarifa Ofisi ya Mkoa,kuchelewa au kushindwa kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa Msajili wa Mashirika, pamoja na kutohuisha taarifa zao katika mfumo wa Nis mfano mtu mmoja kuwa na mashirika zaidi ya moja na kusababisha kupunguza umakini.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaConGO) Mkoa wa Shinyanga Bakari Juma,akisoma Risala ya Mashirika hayo,amesema wanaahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii, pamoja na kulinda mila na desturi za Mtanzania.

Amesema changamoto kubwa ambayo inawakabili kwa sasa ni ukosefu wa vyanzo vya ndani ya mapato, na kutegemea wafadhili.

TAZAMA PICHA👇👇
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni akizungumza.
Afisa Maendeleo wa Mkoa wa Shinyanga Bestina Gunje akizungumza.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaConGO) Mkoa wa Shinyanga Bakari Juma akizungumza.
Picha za pamoja ikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464