` WAZIRI RIDHIWANI KIKWETE AWAKARIBISHA WANANCHI KUTEMBELEA BANDA LA MKOA WA SHINYANGA KWENYE MAONESHO YA SABASABA

WAZIRI RIDHIWANI KIKWETE AWAKARIBISHA WANANCHI KUTEMBELEA BANDA LA MKOA WA SHINYANGA KWENYE MAONESHO YA SABASABA

WAZIRI RIDHIWANI KIKWETE AWAKARIBISHA WANANCHI KUTEMBELEA BANDA LA MKOA WA SHINYANGA KWENYE MAONESHO YA SABASABA

RS SHINYANGA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete, ametoa wito kwa wananchi wote wanaotembelea Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutembelea Banda la Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kupata huduma, bidhaa na taarifa za fursa mbalimbali zinazopatikana katika Mkoa.
Mhe. Ridhiwani alitoa wito huo alipofanya ziara katika banda hilo lililopo mkabala na Banda la TANESCO, huku akiipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa uratibu mzuri, usimamizi makini na ushiriki wa hali ya juu katika maonesho hayo.

Katika ziara hiyo, Waziri Ridhiwani aliambatana na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi, ambapo walipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali ndani yakiwemo yale kutoka Halmashauri zote za Shinyanga.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri mliyoifanya katika kuandaa banda hili. Bidhaa mlizozileta, huduma mnazotoa na namna mnavyowasiliana na wafanyabiashara wengine hakika ni ya kiwango cha juu na hii ni fursa nzuri kwa wafanyabiashara kujifunza na kunufaika,” alisema Mhe. Ridhiwani.

Kwa upande wake, Mhe. Patrobas Katambi aliupongeza uongozi wa Mkoa wa Shinyanga pamoja na wafanyabiashara wote walioshiriki kwa juhudi kubwa waliyoonyesha katika kutangaza bidhaa, huduma na fursa za kiuchumi zinazopatikana mkoani humo.
“Ushiriki wenu ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya kuutangaza Mkoa wa Shinyanga, ni hatua muhimu katika kujitangaza, kuzitangaza bidhaa na huduma na kukuza uchumi wa ndani na kuongeza ajira kwa vijana,” alisema Mhe. Katambi.

Banda la Mkoa wa Shinyanga linabeba dhima ya kuonesha mafanikio ya Mkoa katika Sekta mbalimbali zikiwemo viwanda vidogo, kilimo, biashara, utalii na huduma za kijamii, kuzitangaza fursa za kiuwekezaji zilizopo na hii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera na mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464