
Maadhimisho hayo yana lengo la kukuza na kuimarisha kada ya habari nchini na kusisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na Sheria mpya na rafiki yenye kusimamia mazingira salama kwa waandishi wa habari hasa kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Msemaji mkuu wa shughuli ambae pia ni Mjumbe wa Kamati ya Wataalamu wa masuala ya Habari (ZAMECO) ndugu Salim Said Salim amesema ni jambo la kusikitisha na kutia unyonge kuona kuwa imechukua muda mrefu kupatikana kwa sheria bora ya habari ambapo sheria nyengine zinachukuwa muda mchache kufanyiwa marekebisho.
“Tunashuhudia sheria nyingi zikipitishwa katika Baraza la Wawakilishi, ila sheria ya habari imechukua zaidi ya miaka 20 hali inayoifanya tasnia habari kuwa kama watoto yatima ambao hatuna msaada kwa baba wala kwa mama’’ ameelezea mwandishi huyo mkongwe, Salim Said.
Aidha ameziomba mamlaka husika kuhakikisha wanasimamia ukweli wakati wanapoahidi upatikanaji wa sheria ya habari kwani kufanya hivyo ni kuwavua waandishi wa habari katika janga zito la ufanyaji wa kazi za kuhabarisha umma kwa kutoa taarifa zilizo sahihi katika mazingira salama.
Akizungumza kwa niaba ya katibu mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mratibu wa (MCT, Zanzibar) Ziada Ahmed Kilobo amesema usalama wa wandishi wa habari ni suala la muhimu hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu ambapo Serikali inajukumu la kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi ya kuhabarisha jamii kwa ufasaha na bila ya vitisho.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar ndugu Salum Ramadhan amesema changamoto ya habari ipo njiani kutatuliwa ili kuwawekea waandishi wa habari mazingira mazuri ya kazi, sambamba na sera ya habari ambayo itazinduliwa hivi karibuni.
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) Dkt Mzuri Issa amesema pamoja na waandishi kuwa na wajibu wa kuandika habari kwa weledi na kuzingatia maadili lakini nao wanayo haki ya kupata sheria ya habari inayotetea maslahi yao.
“Sote ni wataalamu na tunafanya kazi kwa kuzingatia hilo lakini lazima tupatiwe haki yetu ya kuwa na sheria nzuri ya habari, kufuatilia michakato ya sheria, kupewa ulinzi pamoja na kutopewa vitisho na kufanya kazi kwa usawa na ukweli.
Siku ya Uhuru wa Habari Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Mei ambapo kwa upande wa Zanzibar kauli mbiu inasema “Sheria nzuri ya Habari ni chachu ya uchaguzi ulio huru na wa haki”.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano na Utetezi













