USIKU WA WAUGUZI MANISPAA YA SHINYANGA WAFANA,KATAMBI ANOGESHA SHEREHE
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
WAUGUZI wa Manispaa ya Shinyanga,wamefanya sherehe kwa ajili ya kusherehekea kuadhimisha siku ya wauguzi duniani kwa kumuenzi muuguzi wa kwanza duniani Florence Nightingale.
Sherehe hizo zimefanyika jana katika ukumbi wa Lyakale,huku Mgeni Rasmi akiwa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na Watu wenye ulemavu.
Akisoma risala ya wauguzi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Judith Masalu, amesema wameadhimisha sherehe hiyo, ili kumuenzi mwanzilishi wa huduma ya uuguzi duniani Florence Nightingale,ambaye alileta mageuzi makubwa kwenye kada ya uuguzi kwa kutumia muda wake mwingi kuhudumia wagonjwa kwa moyo wa huruma na upendo.
Amesema siku hiyo ya wauguzi duniani ilianzishwa ili kuongeza uelewa wa wajibu na majukumu ya wauguzi pamoja kuona umuhimu wa kutimiza mahitaji ya wauguzi duniani kote.
Amesema kwamba, wauguzi wakitumiwa ipasavyo pamoja na kuwekewa mazingira mazuri ya utendaji kazi na kuboreshewa maslahi yao,wanamchango mkubwa katika kuimarisha afya ya jamii.
“Wauguzi wamekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga,kupunguza magonjwa mbalimbali kama vile malaria,kifua kikuu,polio na maambukizi ya virusi vya ukimwi, hivyo sisi ni nguzo ya kuimarisha afya za wananchi,”amesema Judith.
Aidha,amesema licha ya serikali kuboresha huduma za afya,lakini kada hiyo ya uuguzi bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya idadi ndogo ya wauguzi ukilinganisha na idadi ya wagonjwa, baadhi ya vituo kutotoa fedha kwa ajili ya sare za kazi kwamujibu wa muongozo.
Ametaja changamoto nyingine ni upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali kwenye vituo na hivyo kusababisha wauguzi kufanya kazi zilizo nje na taaluma yao,pamoja na kudai malipo ya muda wa ziada ya kipindi chote cha utoaji wa huduma katika kambi za magonjwa ya mlipuko kama vile COVID-19.
Pia, wameahidi kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili,miongozo,sheria,kanuni na miiko ya taaluma yao, ili kuimarisha afya za wagonjwa,huku wakilaani vikali tabia ya baadhi ya wauguzi wachache ambao wamekuwa hawafuati miongozo hiyo na kuharibu taswira ya uuguzi kwa jamii.
Katika hatua nyingine,wamempongeza Mbunge Katambi kwa kuendelea kutunisha mfuko wa SACCOS yao kwa kutoa tena kiasi cha sh.milioni 2,ambapo mwaka jana alitoa sh.milioni 1.
Naye Mgeni Rasmi Mbunge Katambi, amesema kwamba serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan inatambua mchango mkubwa ambao unafanywa na wauguzi katika kuimarisha afya za wananchi,na kwamba itaendelea kuboresha huduma za afya pamoja na kulinda maslahi yao.
Amesema kwa changamoto zote ambazo zimewasilishwa watazifanyia kazi kwa vitendo, kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze, ambaye ni Mkurugenzi anayejali maslahi ya Watumishi wake.
“Serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka minne,imeboresha sana huduma za afya, mfano hapa shinyanga mbali na kukamilisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Manispaa,zimejengwa Zahanati mpya 7,Vituo vya Afya kikiwamo cha Ihapa, na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa ikiwamo EX-RAY Digital Mashine,”amesema Katambi.
Amesema kwa upande wa ajira,kwamba tayari awali serikali ilitoa ajira 146 na wanatarajia tena kuajiri watumishi wapya 54 wakiwamo wauguzi, kutokana na serikali kutambua kwamba, afya ndiyo mtaji namba moja kwa wananchi.
Katika hatua nyingine Mbunge Katambi,alitoa msamaha kwa Madaktari na Wauguzi ambao walikuwa wakikatwa mishahara yao kutokana na kutumikia adhabu ya makossa mbalimbali kazini kwa mujibu wa sheria na miongozi ya kazi, kwamba Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga aanze kuwalipa mishahara kamili.
Naye Mkurugenzi huyo Alexius Kagunze, amesema atalifanyia kazi suala hilo kuanzia siku ya Jumatatu.
Katika sherehe hiyo zilitolewa zawadi mbalimbali wakiwamo Watumishi Hodari na Wauguzi Wastaafu.
Aidha,kila ifikapo Mei 12 kila mwaka Wauguzi kote duniani usherehekea siku ya wauguzi kwa kumuenzi muuguzi wa kwanza duniani Florence Nightingale,ambaye alizaliwa kwenye mji wa Florence nchini Itali mwaka 1820.
TAZAMA PICHA👇👇
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu akizungumza.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Shinyanga Dk.Elisha Robert akizungumza.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Elexius Kagunze akizungumza.
Muuguzi Judith Masalu akisoma Risala.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze pamoja na Muuguzi Judith Masalu wakikata keki kwenye sherehe hiyo.
Sherehe ikiendelea.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464