MADIWANI SHINYANGA WALALAMIKIA HUDUMA MBOVU YA UMEME,KATA YA MWAMALILI HAINA UMEME HATA KIJIJI KIMOJA

MADIWANI SHINYANGA WALALAMIKIA HUDUMA MBOVU YA UMEME KATA YA MWAMALILI HAINA UMEME HATA KIJIJI KIMOJA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, wamelalamikia huduma mbovu ya umeme katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo, huku baadhi ya kata zikikosa kabisa umeme hadi kwenye vijiji vyake vyote.
Malalamiko hayo yalitolewa leo, Mei 7, 2025, katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo, wakati wa kujadili taarifa ya Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga.

Wakichangia taarifa hiyo, madiwani hao wamesema huduma ya umeme kwa wananchi haifanyiwi maboresho ya kuridhisha, huku maeneo mengi yakikumbwa na kukatika kwa umeme mara kwa mara, na baadhi ya kata kutokuwa na umeme hata kijiji kimoja.
Diwani wa Kata ya Mwamalili James Matinde,amesema hawana sababu ya kuipongeza TANESCO, kwa kuwa hakuna kijiji hata kimoja katika kata yake kilichounganishwa na umeme.

Naye Diwani wa Kata ya Chibe John Kisandu,amesema kuwa Mtaa wa Mwamapalala umekuwa hauna umeme kwa muda mrefu, licha ya maombi yaliyowasilishwa mara kadhaa, huku akidai wamekuwa wakipewa ahadi zisizotekelezwa.
“Kama haiwezekani mtaa huo wa Mwamapalala kupelekewa huduma ya umeme, basi ni vyema tuambiwe wazi ili wananchi waendelee kutumia vibatari,” amesema Kisandu.

Diwani wa Kizumbi Rubeni Kitinya, naye alilalamikia kwamba kwenye baadhi ya maeneo ya huduma za kijamii hayana umeme kwa kipindi kirefu ikiwamo Zahanati ya Lyandu.
Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum,Pica Chogelo, alilalamikia kukatika kwa umeme mara kwa mara, hasa nyakati ambazo michezo ya mpira inapaswa kuanza.

Naye Diwani wa Mwawaza Juma Nkwambi,alilalamikia tatizo la nguzo za mradi wa kijiji cha Ishoshandili, kwamba kulikuwa na nguzo 170 kwenye mradi huo,na kudai kwamba nguzo zilizofika ni 75 tu, huku akiingiwa na hofu huenda nguzo 95 zilizobaki zimeuzwa na kuhoji ziko wapi.
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Seraphine Lyimo, akijibu hoja hizo za madiwani, amesema kuwa changamoto zote hizo zitafanyiwa kazi pamoja na kufika kwenye maeneo husika ili kuona hali halisi, huku akionyesha kushitushwa na Kata ya Mwamalili kutokuwa na umeme hata kijiji kimoja.

Amesema kuwa yeye ni mgeni,na kwamba katika utatuzi wa changamoto hizo atafanya ziara kwa kila eneo, huku akiwatoa hofu madiwani, kuwa kuna mradi mkubwa wa umeme unakuja chini ya wafadhili,na Rais Samia amesha saini,na kila eneo litafikiwa na huduma hiyo ya umeme.

Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko, amewataka madiwani kushirikiana na Meneja wa TANESCO, pale atakapofika katika maeneo yao ili kurahisisha utatuzi wa kero hizo.

TAZAMA PICHA👇👇
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akizungumza.
Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Zamda Sahabani akizungumza.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze akizungumza.
Diwani wa Mwamalili James Matinde akilalamikia Kata hiyo kutokuwa na umeme hata Kijiji Kimoja.
Diwani wa Lubaga Rubeni Dotto akilalamikia huduma ya umeme.
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Seraphine Lyimo akijibu malalamiko ya madiwani juu ya huduma ya umeme.
Kikao cha Baraza la Madiwani kikiendelea.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464