MADIWANI SHINYANGA WALALAMIKIA UBOVU WA BARABARA,TARURA WALIA NA UFINYU WA BAJETI
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MADIWANI wa Manispaa ya Shinyanga,wamelalamikia hali mbaya ya barabara katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo,huku wakitaka hatua madhubuti zichukuliwe na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), ili kuokoa wananchi wanaoteseka kutokana na miundombinu mibovu.
Naibu Meya wa Manispaa hiyo Zamda Shabani,amesema hali ya barabara ni mbaya mno,na kuisihi TARURA kuwa, mara tu wanapopata fedha, waanze kukarabati barabara zilizo katika hali mbaya zaidi.
Diwani wa Viti Maalum,Pica Chogelo, amesisitiza umuhimu wa kupewa kipaumbele barabara zinazohudumia taasisi muhimu za kijamii kama shule na zahanati,hata kama fedha ni chache.
Naye Diwani wa Lubaga Rubeni Dotto,alipendekeza halmashauri inunue mtambo wake wa kutengenezea barabara ili kupunguza utegemezi kwa TARURA.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko, naye alikiri kuwa barabara ni mbaya, na kuwataka madiwani kuacha kulalamika sana, ikiwa kwani chanzo kinajulikana kuwa niufinyu wa bajeti.
Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Shinyanga,Mhandisi Kulwa Maige, alifafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 waliidhinishiwa sh. bilioni 2.9, huku bajeti ya matengenezo ya barabara ikiwa Sh. bilioni 1.4, lakini mpaka sasa wamepokea Sh. milioni 85.4 pekee.
“Ufinyu wa bajeti ndiyo kikwazo kikuu katika matengenezo ya barabara ukilinganisha na urefu wa mtandao wa barabara tulio nao, katika utatuzi wa tatizo hili tunaomba halmashauri iwe inatenga fedha kupitia mapato yake ya ndani ili kusaidia ukarabati wa barabara, badala ya kuitegemea TARURA pekee,” amesema Mhandisi Maige.
TAZAMA PICHA👇👇
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akizungumza kwenye kikao cha baraza.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Zamda Shabani akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Shinyanga Mhandisi Kulwa Maige akiwasilisha taarifa ya TARURA.
Kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Shinyanga kikiendelea.
Madiwani wakiendelea na kikao cha Baraza.