Header Ads Widget

RIPOTI MAALUM; UCHAFUZI WA MAZINGIRA KWA KUKOSA VYOO UNAVYOWEKA REHANI AFYA ZA WACHIMBAJI WADOGO WA DHAHABU BUTIAMA


Wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Mgodi wa Sirorisimba Butiama mkoani Mara.
Wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Mgodi wa Sirorisimba Butiama mkoani Mara.

Uchafuzi wa Mazingira kwa kukosa vyoo unavyoweka rehani afya za wachimbaji wadogo wa dhahabu Butiama

Na Marco Maduhu, aliyekuwa BUTIAMA

UCHIMBAJI mdogo wa madini umekuwa ukitoa ajira nyingi kwa wananchi wakiwamo vijana na wanawake, lakini baadhi ya Machimbo kumekuwapo na tatizo la kutozingatiwa suala la afya na usafi wa mazingira, kwa kukosa vyoo na kulazimika wachimbaji kujisaidia vichakani.

Mwandishi wa Makala hii ametembelea baadhi ya Migodi Midogo ya Uchimbaji Madini ya dhahabu iliyopo halmashauri ya wilaya ya Butiama mkoani Mara, na kukuta Migodi mingine haina vyoo kabisa kwa ajili ya kujisaidia wachimbaji, huku mengine ikiwa na vyoo ambavyo siyo bora ‘vyakuzugia’.

Wilaya ya Butiama ina Migodi midogo ya uchimbaji madini ya dhahabu ukiwamo Mgodi Sirorisimba, Magunga, Nyasirori, Nyamikoma, Biatika, Nyanza na Migodi mingine midogo ambayo inachipukia.

Mgodi ambao umekutwa hauna vyoo kabisa ni Mgodi wa Sirorisimba, na wachimbaji wamekuwa wakijisaidia vichakani kwa kuchafua Mazingira na kuhatarisha afya zao.

Sheria ya Mazingira No 20 ya mwaka 2004, inazungumzia suala la udhibiti wa uchafuzi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya shughuli za binadamu yakiwamo na machimbo ya madini.

Sheria ya madini No 14 ya mwaka (2010) inazungumzia juu ya kufutwa kwa lesseni iwapo tathimini ya athari za mazingira itakataliwa, na katika mkataba wa utoaji wa lesseni ya uchimbaji madini kuna vipengele vya utunzaji wa mazingira, lakini katika Migodi midogo ya Butiama baadhi imekiuka mkataba huo na kushindwa kutunza mazingira.

Mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu katika Mgodi wa Sirorisimba eneo lenye Lesseni ya Mama Shida Josephine Chacha, anasema katika machimbo hayo hakuna vyoo na wamekuwa wakijisaidia vichakani haja zote kubwa na ndogo.

Anasema wao kama wanawake ni aibu kujisaidia vichakani wakichangamana na vijana na kushusha utu wa mwanamke, lakini kutokana na utafutaji wa riziki wameshazoea hali hiyo.

“Hapa Mgodini hakuna vyoo, watu wote unaotuona hapa si vijana wala wanawake, wote tunakwenda kujisaidia vichakani, huo ndiyo ukweli hakuna kuficha sababu tunaodhalilika ni sisi,”anasema Josephine.

Mchimbaji mwingine mdogo kwenye Lesseni ya Serikali ya Kijiji cha Sirorisimba Nyamhanga Marwa, anasema eneo hilo nalo halina vyoo na miaka yote wamekuwa wakijisaidia vichakani na kwenye mapori ya mgodi huo.

Anasema licha ya eneo ambalo wanafanya shughuli za uchimbaji madini kumilikiwa na Serikali ya Kijiji cha Sirorisimba, lakini nalo halina vyoo kama maeneo mengine, na kuhoji kama tu Serikali haitambui umuhimu wa vyoo je watu baki itakuwaje.

“Ukosefu wa vyoo kwenye maeneo haya ya machimbo ya madini ni hatari sana, sababu kuendelea kujisaidia vichakani ni kutapanya vinyesi hovyo na katika kipindi hiki cha mvua kunaweza kutokea magonjwa ya mlipuko,”anasema Marwa.

Nyandoge Mwita ambaye naye ni mchimbaji mdogo katika Mgodi huo wa Sirorisimba, anawaomba wadau wa mazingira pamoja na vyombo vya habari, kupaza sauti na kutoa elimu hasa kwa wamiliki wa Lesseni wazingatie afya za watumishi wao na kuwajengea vyoo na siyo kwenda vichakani.

Msimamizi wa machimbo katika Lesseni ya Mama Shida Dorica Kitomari ambaye pia ni Mhasibu, anakiri eneo hilo halina choo na sasa wameshaanza mpango wa kuchimba choo ili wachimbaji wao wasiende kujisaidia tena vichakani.

“Eneo hili hatuna choo kilianguka na sasa tunachimba kingine hicho hapo unaona vijana wapo kazini,”anasema Dorica.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Sirorisimba Ibrahimu Mniko, anasema Machimbo yaliyopo kwenye kijiji hicho hayana vyoo, na hata eneo lenye Lesseni ya kijiji nalo hakuna vyoo, na kukiri kuwa wachimbaji hujisaidia vichakani na kwenye mapori ya mgodi huo.

Anasema suala la vyoo kwenye machimbo ni muhimu sababu kuna muingiliana wa watu wengi, na nihatari kutokea magonjwa ya mlipuko kikiwamo kipindupindu.

“Tatizo hapa ni ukosefu tu wa elimu ya umuhimu wa kuwa na vyoo kwenye machimbo, lakini wachimbaji wakielimishwa vizuri watajenga vyoo sababu ni muhimu kwa afya zao, na katika eneo letu la Serikali ambalo lina lesseni ya uchimbaji tutajitahidi kujenga choo ili tutoe mfano kwa wachimbaji wengine,”anasema Mniko.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Sirorisimba Masunga Magati, anasema Mgodi huo una miaka zaidi ya 10, na hakuna idadi kamili ya wachimbaji waliopo sababu wamekuwa wakiingia na kutoka, lakini watu walio na Lesseni wapo Sita likiwamo na eneo la kijiji.

“Kila mwenye Lesseni katika Mkataba wake anapaswa kutunza mazingira na kujenga vyoo, lakini waliona vyoo ni wale wenye maeneo ya uchenjuaji tu (ukamataji dhahabu), lakini kwenye maduara ya kuchimba madini hakuna vyoo kabisa, itabidi Serikali ya kijiji tushirikiana na watu wa mazingira kutoa elimu ujenzi wa vyoo,”anasema Magati.

Meneja wa Mgodi wa Irasanilo Gold Mine ambao wana Lesseni katika eneo la Machimbo ya Magunga Robert Lucas. anasema wao walijiwekea Sheria ndogo, kuwa marufuku mwekezaji kufanya shughuli za uchimbaji madini bila ya kuwa na choo, pamoja mchimbaji akijisaidia vichakani akikamatwa anatozwa faini ya Sh.50,000 na mwekezaji akikutwa hana choo faini Milioni 5.

Afisa Taka na Usafi wa Mazingira Halmashauri ya wilaya ya Butiama Karani Ruhumbika, anasema matumizi ya vyoo kwenye Migodi ya Madini wilayani humo siyo mkubwa, sababu baadhi ya migodi hakuna vyoo kabisa, na mingine ina vyoo lakini siyo bora.

Anasema, Serikali imekuwa ikijitahidi kutoa elimu mara kwa mara kwa wachimbaji kujenga vyoo lakini muitikio wake umekuwa mdogo, sijui mpaka yatokee maafa ndipo wajenge.

“Mfano katika Mgodi wa Magunga, wachimbaji walichimba vyoo wenye mara baada ya kutokea kipindupindu mwaka (2014) japo nao vyoo vya siyo imara lakini afadhali kuna vyoo, siyo kama Mgodi wa Sirorisimba ambao hauna vyoo kabisa,”anasema Ruhumbika.

“Tulibaini ubishi wa kutojenga vyoo hasa kwenye maeneo ya maduara ya uchimbaji madini, sababu wao ni watu wa kuhamahama wanafuata dhahabu ilipo ndiyo maana hawaoni umuhimu wa vyoo na kujisaidia vichakani, kitendo ambacho ni hatari sababu maeneo hayo kuna watu wanaishi,”anaongeza Ruhumbika.

Anasema wao kama Serikali hawatachoka kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kujenga vyoo kwenye maeneo ya machimbo, na anawasihi wachimbaji wadogo wafuate maelekezo ya wataalamu kutunza mazingira siyo mpaka utokee mlipuko wa magonjwa.

Afisa Afya Halmashauri ya wilaya ya Butiama Mohamed Selemani, anasema tatizo la ukosefu wa vyoo kwenye baadhi ya machimbo wilayani humo lipo, na wamekuwa wakitoa elimu kwa wachimbaji kwamba wajenge vyoo lakini muitikio wake umekuwa mdogo na kushindwa kutekeleza maelekezo ambayo wanayatoa.

Anasema, wanachokipanga kwa sasa ni kutunga sheria ndogo ambayo itaibana Migodi yote kujenga vyoo, na watakao shindwa kutekeleza sheria hizo watatozwa faini.

“Migodi kutokuwa na vyoo ni hatari sana kutokea magonjwa ya mlipuko, kuna kipindi fulani Mgodi wa Magunga ulifungwa sababu ya ukosefu wa vyoo na kulikuwa na wachimbaji wengi sana, lakini leo hii wanavyoo na hili tutalifanya kwenye migodi mingine ili nao wajenge vyoo,”anasema Selemani.

Kaimu Mganga wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama Dk. Sunday Malulu, anasema Migodi kukosa vyoo kiafya ni hatari, na kubainisha kuwa suala hilo itabidi waandike barua kwenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Butiama, ili kuweka msisitizo kwa wachimbaji kujenga vyoo na kuwabana watendaji wa Kata kulisimamia hilo.

“Kesi za wachimbaji kuugua magonjwa ya matumbo zipo, lakini katika Hospitali ya wilaya ya Butiama hatuna takwimu sahihi, sababu wengi hutibiwa kwenye Zahanati pamoja na wengine kwenda Hospitali za Musoma kutokana na Migodi mingine kuwa karibu na Musoma,”anasema Dk. Malulu.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama Revocatus Rutunda, anasema katika wilaya hiyo ya Butiama kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa Mazingira kutokana na kuchipukia kwa Migodi mingi midogo midogo.

Anasema katika Migodi ambayo ina wachimbaji wengi ukiwamo Mgodi wa Magunga na Sirorisimba ambao hauna vyoo kabisa, tayari Serikali imeshaanza ujenzi wa vyoo vya kulipia na ujenzi wake upo katika hatua ya umaliziaji, huku wakiendelea kutoa elimu ya hamasa ya ujenzi wa vyoo kwenye machimbo yote.

“Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kuna Migodi mingi midogo ambayo inachipukia hivyo hatari ya uharibifu wa mazingira ni mkubwa sana, tutakacho kifanya kama Serikali ni kutunga Sheria ndogo za usimamizi wa mazingira,”anasema Rutunda.

“Kuna vijiji viwili vya Kamgendi na Lyamisanga wao walitunga Sheria ndogo mara baada ya kuona uharibifu wa Mazingira katika maeneo yao umekuwa mkubwa, na sisi tukazichukua tukampatia Mwanasheria wetu akazipitia na kuziwalisha kwenye vikao vya kamati zikabailikiwa na kuanza kutumika,”anaongeza Rutunda.

Meneja wa Baraza la Taifa la uhifadhi na usimamizi wa mazingira Kanda ya Ziwa (NEMC) Jerome Kayombo, anasema suala hilo la ujenzi wa vyoo kwenye migodi midogo linaweza tekelezwa na halmashauri husika kupitia Maofisa Mazingira.

“Sheria ya usimamizi wa mazigira ni kupiga faini tu, lakini hilo la ukosefu wa vyoo machimboni linaweza kudhibitiwa ngazi ya halmashauri, wakishindwa ndiyo tunakuja sisi kusimamia sheria”anasema Kayombo.

“Lakini wiki ijayo nitatuma Maofisa wangu kutoka hapa NEMC waungane na Maofisa Mazingira kutembelea Migodi hiyo ya Butiama, na kuhamasisha ujenzi wa vyoo, na watakaokiuka sasa ndipo tutasimamia sheria na kuwatoza faini,”anaongeza Kayombo.


Chama cha Wanasheria watetezi wa Mazingira kwa vitendo (LEAT), wanasema suala la ukosefu wa vyoo kwenye badhi ya Migodi Butiama, Serikali inapaswa kuliangalia kwa macho matatu ili baadae kusije tokea maafa makubwa ya mlipuko wa kipindupindu ndipo waanze kukimbizana na kumtafuta mchawi nani.

Ofisa Miradi wa (LEAT) Clay Mwaifani, anasema Serikali inapaswa kusimamia ipasavyo sheria za madini, Mazingira na ajira, sababu wachimbaji wanapofanya kazi bila kuwapo na huduma muhimu kama choo huo ni ukiukaji wa sheria na wanapaswa kuchukuliwa hatua.

“Suala hili la wachimbaji kukosa vyoo na kujisaidia vichakani ni ukosefu wa uwajibikaji kwa viongozi na mamlaka husika ambazo zinasimamia sheria za madini, mazingira, na usalama mahala pa kazi, hapa kuna uzembe mahali unafanyika,”anasema Mwaifani.

Post a Comment

0 Comments