Header Ads Widget

TAIFA STARS YALAZIMISHWA SARE YA 1-1 NA CONGO DR MBELE YA WAZIRI BASHUNGWA IKIMUAGA BEKI AGGREY MORRIS

Wachezaji wa Taifa Stars wakimpongeza Ayoub Lyanga baada ya kuifungia timu hiyo bao la kusawazisha dhidi ya Congo DR leo katika mchezo wa kirafiki uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam (Picha na TFF

Na Damian Masyenene
TIMU ya Taifa 'Taifa Stars' imelazimishwa sare ya bao 1-1 na wageni wao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Congo DR) katika mchezo wa kirafiki wa kujipima uwezo uliopigwa leo kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam ukishuhudiwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Innocent Bashungwa, naibu wake, Abdallah Ulega na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Mchezo huo ulikuwa maalum kwa ajili ya kikosi cha Taifa Stars kujipima ubavu na kujiweka tayari kwa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) yanayotarajiwa kufanyika hivi karibuni nchini Cameroon.

Katika mchezo huo, Wageni Congo DR ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 18 ya mchezo kupitia kwa Fiston Mayele,huku Stars wakisawazisha mnamo dakika ya 51 kupitia kwa Ayoub Lyanga akiunganisha kwa kichwa krosi safi ya Ditram Nchimbi

Mabadiliko mengine yalikuwa ya Baraka Majogoro aliyechukua nafasi ya Ndemla, Farid Musa akichukua nafasi ya Ayoub Lyanga na Israel Patrick akiingia badala ya Lucas Kikoti.

Kikosi cha Stars kilichoanza katika mchezo huo ni Juma Kaseja, Yasin Mustapha, Shomari Kapombe, Ame Ally, Aggrey Morris, Feisal Salum, Said Ndemla, Lucas Kikoti, Deus Kaseke, Ayoub Lyanga na Adam Adam.

Mchezo huo pia ulitumika kumuaga rasmi Beki Kisiki wa Taifa Stars, Aggrey Morris mwenye umri wa miaka 36, ambaye alikuwa nahodha wa kikosi hicho leo akicheza kwa dakika takribani tano. Morris ambaye pia anaitumikia Azam FC alijiunga na Stars mnamo mwaka 2010 akitajwa kuitumikia timu hiyo katika mechi 35, ambapo amestaafu rasmi kuichezea timu ya taifa.

Rais wa TFF Wallace Karia akimkabidhi Aggrey Morris jezi iliyosainiwa na Wachezaji, benchi la Ufundi na viongozi ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya beki huyo kustaafu kuchezea timu ya Taifa “Taifa Stars”
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bushungwa akimkabidhi Aggrey Morris hundi ikiwa ni sehemu ya zawadi ya beki huyo kustaafu kuchezea timu ya Taifa “Taifa Stars”


Post a Comment

0 Comments