Header Ads Widget

ASKARI POLISI WALIOMKERA RAIS MAGUFULI WAONDOLEWA

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro

INSPEKTA Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro ametekeleza agizo la Rais John Magufuli la kuwaondoa katika vituo vyao vya kazi polisi wa Kituo cha Mlandizi mkoani Pwani, kwa uzembe na kutowajibika ipasavyo.

Hali hiyo ilisababishwa na kuhujumiwa kwa miundombinu ya Reli ya Kisasa (SGR) katika mkoa huo. Kwa sasa SGR inajengwa kutoka Dar kwenda Moro hadi Dodoma.

Jana HabariLEO lilitaka kujua uhalisia wa jibu alililotoa IGP Sirro kwa Rais Magufuli, alipoulizwa kama amekwishawaondoa askari hao Mlandizi mkoani Pwani. Hayo yalijiri katika hafla ya kuwaapisha mawaziri na naibu mawaziri, iliyofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma juzi.

Akifafanua hali hiyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime, alisema tayari viongozi hao walikwishaondolewa Mlandizi na nafasi zao kupangiwa wengine.

Kwa mujibu wa Misme, katika mabadiliko hayo, IGP Sirro aliwahamisha aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mlandizi (OCD), Severine Msonda na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mlandizi (OCS), Michael Kaniki kwenda Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani.

Alisema Mkuu wa Polisi Wilaya ya Gairo, Julieth Lyimo sasa anakuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mlandizi huku Joel Mkuche aliyekuwa Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani atakuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mlandizi.

Akithibitisha mintarafu taarifa za kuwapo mabadiliko katika uongozi wa Kikosi cha Reli, Misime alisema IGP Sirro amemhamisha aliyekuwa Kamanda wa Kikosi hicho, Pudensiana Protas kwenda Makao Makuu ya Polisi kuwa Ofisa Mnadhimu katika Kamisheni ya Operesheni na Mafunzo.

Nafasi ya Protas, imechukuliwa Ofisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Sebastian Mbutta.
TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807