Header Ads Widget

LISSU AZINDUA KAMPENI KANDA YA SERENGETI, ATANGAZA NEEMA KWA WAKULIMA NA WAFUGAJI


Mgombea Urais kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu pamoja na Mgombea mwenza wa chama hicho, Salum Mwalimu wakiwapungia wananchi wakati walipowasili kwenye uwanja wa Joshoni Mjini Shinyanga kuzindua kampeni za chama hicho kwa Kanda ya Serengeti leo Septemba 2, 2020. Picha zote na Marco Maduhu

Na Damian Masyenene - Shinyanga
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameendelea na uzinduzi wa kampeni zake katika kanda mbalimbali za chama hicho nchini, ambapo leo Septemba 2, 2020 ilikuwa zamu ya Kanda ya Serengeti inayojumuisha mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara.

Lissu amefanya uzinduzi huo mjini Shinyanga yalipo makao makuu ya kanda hiyo katika uwanja wa Joshoni akisindikizwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Mgombea Mwenza, Salum Mwalimu, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, Esther Matiko, Mgombea Ubunge Jimbo la Bunda Mjini, Esther Bulaya na Mgombea Ubunge jimbo la Shinyanga Mjini, Salome Makamba pamoja na baadhi ya wagombea ubunge na udiwani katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Shinyanga.

Kabla hajapanda jukwaani kuzindua kampeni hizo na kuzungumza na maelfu ya wafuasi wa chama hicho waliofurika uwanjani hapo kumshuhudia, Lissu amefanyiwa maombi na dua maalum, kuvalishwa vazi maalum, kukabidhiwa mkuki wa ushindi na usinga na kiti cha kifalme na wazee wa kabla la Kisukuma.
Tundu Lissu akiwapungia wananchi baada ya kusimikwa uchifu na wazee wa Kisukuma

Akinadi ilani za chama chake na sera kwa wananchi hao, Tundu Lissu amesisitiza kwamba Serikali ya chama hicho itakuwa ya haki na itakayoponya majeraha ambayo wananchi wamekuwa nayo katika sekta mbalimbali ikiwemo uvuvi, kilimo na ufugaji.

Akirejea kaulimbiu ya ilani ya chama chake inayosisitiza Uhuru, Haki na Maendeleo ya Watu, Tundu Lissu   amesema atahakikisha wakulima wanapata haki kwa kutokopwa mazao yao, huku pia akibainisha kuwa Serikali yake itatengeneza utaratibu utakaowezesha wafugaji kuchunga kwenye hifadhi wakati wa shida ya malisho na maji.

"Serikali ya Chadema itapiga marufuku mtu yeyote, taasisi ama kikundi cha watu kitakachokopa mazao ya Wakulima, tunataka wakulima wetu wapate haki yao kwa kuuza mazao kwa bei halali itakayoleta nafuu kwao.

"Pia hatutakubali mfugaji akamatwe mifugo yake, ifilisiwe ama akamatwe," alisema 

Vilevile, Lissu amekazia kwa kueleza kwamba kitu cha kwanza ambacho Serikali yake itafanya itakapoingia madarakani ni kurudisha mahusiano mema na mataifa mengine (duniani) na kuweka utaratibu mzuri wa watu kufanya biashara kwa uhuru bila kukandamiza watu.

Naye Mgombea Mwenza wa Chadema, Salum Mwalimu ameeleza kuwa miongoni mwa mambo mema watakayoyafanyia kazi wakiingia madarakani ni pamoja na wakulima na wafugaji kutumia mifugo yao kuweka dhamana ya kupata mikopo kuendeleza huduma nyingine.

"Ndugu zangu tuwe makini sana, uchaguzi huu siyo ushabiki wa Simba na Yanga, huu ni mustakabali wa maisha yetu tusifanye makosa tuchague haki," alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amesema siku takribani 55 zilizobaki kuelekea uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu wafuasi wa chama hicho wazitumie kutafakari na kufanya uamuzi na zisiwe siku za kufanya masihara.

"Awamu hii tusichague Bendera za vyama vyetu bali tuchague mustakabali wa maisha yetu......Kanda ya Serengeti ni Kanda imara, tunaitegemea Sana kwa ushindi mkubwa," alisema.

Awali akihutubia maelfu ya wananchi na wafuasi wa Chadema waliojitokeza kusikiliza sera za chama hicho, Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, John Mnyika amesema kwamba taifa linakwenda kumpata Rais atakayekwenda kusimamia haki ya nchi na maendeleo ya rasilimali katika maeneo mbalimbali, hivyo akawaomba wananchi na wafuasi wa chama hicho kuwapa kura za ushindi madiwani na wabunge wote wa kanda hiyo ili kumsaidia Tundu Lissu kupata wasaidizi makini.


Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu akizungumza na wananchi waliojitokeza leo kwenye uwanja wa Joshoni Mjini Shinyanga kushuhudia uzinduzi wa kampeni za chama hicho kwa kanda ya Serengeti


Mgombea Mwenza wa Chadema, Salum Mwalimu akizungumza na wananchi wakati wa mkutano huo


 Baadhi ya wafuasi wa Chadema wakiwa wamepanda juu ya mti wakati wakishuhudia mgombea Urais kupitia chama hicho, Tundu Lissu akizindua kampeni zake leo mjini Shinyanga


 Wafuasi wa Chadema wakifuatilia zoezi la uzinduzi wa kampeni za chama hicho Kanda ya Serengeti kwenye uwanja wa Joshoni Mjini Shinyanga

Wafuasi wa Chadema wakiendelea kusikiliza sera za viongozi wao kuelekea uchaguzi mkuu

Tundu Lissu akizungumza na wafuasi wa chama hicho leo katika uwanja wa Joshoni mjini Shinyanga