Header Ads Widget

UMMY MWALIMU ALA KIAPO DHIDI YA WANAOMTUKANA MAJUKWAANI

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Tanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ummy Mwalimu (katikati) akizungumza wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa wagombea ubunge na udiwani  wanawake katika semina iliyoandaliwa na Shirika la Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WILDAF) na kuratibiwa na Mkurugenzi wa Shirika la Agri Thamani Foundation, Neema Lugangira (Kushoto) na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Shirika hilo, Rehema Maro

Na Mwandishi Wetu
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Tanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ummy Mwalimu amesema kwamba kamwe hatawajibu wanaomtukana kwenye majukwaa badala yake ataeleza namna atakavyoweza kuwa chachu ya kuleta maendeleo kwa wananchi wakati akipewa ridhaa ya kuwaongoza.

Ummy ambaye pia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ametoa kauli hiyo leo Septemba 2, 2020 wakati wa semina ya uongozi kwa wagombea ubunge na udiwani wanawake iliyoandaliwa na Shirika la Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WILDAF) na kuratibiwa na  Shirika la Agri Thamani Foundation  ikikusudia kusaidia kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za uongozi na maamuzi.

Amesema kwamba atakachokifanya wakati akiendesha kampeni zake za kuwania ubunge jimbo la Tanga, atajikita kwenye kueleza namna atakavyosaidia wananchi kuweza kujikwamua kimaendeleo kwa kuona namna ya kushirikiana nao katika kufikia mafanikio.

“Niseme tu kwamba nitakapokuwa kwenye kampeni sitatumia jukwaa kuwajibu ambao wananitukana badala yake nitajikita kwenye kutangaza maendeleo makubwa na mipango ambayo nitawafanyia wananchi wa Jimbo la Tanga lakini pia niwashukuru wajumbe wa UWT kwa sapoti kubwa kwangu,” amesema.

Hata hivyo amewaomba wanawake wanaowania uongozi kwenye nafasi mbalimbali wasiwe mawakala wa kuwatukana watu ikiwemo kuwadhalilisha wanawake wenzao, huku akiwasihi wanawake hao kubadilika na kutoyashikia mabango maneno yasiyofaa yanayosemwa na wenzao majukwaani.

Ummy amewataka wagombea hao kuhakikisha hawawi mawakala wa kusambaza mambo ya hovyo yanayodhalilisha utu na haki ya wanawake kwa sababu wao ndiyo walezi wa familia na ndiyo watapambanaji ambao wanalea familia hivyo watambue wana umuhimu mkubwa kwenye jamii

“Ndugu zangu tusifanye kampeni za matusi za kudhalilisha wanawake wenzetu kwenye majukwa lakini niwaambie kwamba wakati wa kampeni zangu hawatanisikia nikiwajibu ambao wananitukana badala yake nitajikita kwenye kutangaza namna nitakavyoleta maendeleo,” amesema Ummy Mwalimu.

Vile vile, amewataka wanawake kuhakikisha wanasaidiana, kuacha kuoneana wivu na choyo badala yake washirikiane katika kujiletea maendeleo ambayo yatawasaidia kuweza kujikwamua kiuchumi wao na jamii ambazo zinawazunguka.

Ummy pia ameyaomba mashirika hayo wakati mwengine kuipeleka semina hiyo katika mikoa mingine wanawake kuwa mstari wa mbele kupigania vipaumbele vya wanawake katika afya ya mama na mtoto, elimu kwa watoto wa kike kwa lengo la kuweza kuwakomboa

Awali akizungumza kwenye semina hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la Agri Thamani Foundation, Neema Lugangira amesema wamejikita kutoa elimu kwenye masuala ya lishe na kuhamamisha kilimo lishe.

Ameeleza kuwa mwaka 2018 walianza mchakato maalum wa kisera kuhakikisha agenda hiyo inaingia kikamilifu kwenye ilani ya uchaguzi mafanikio ilani ya uchaguzi ya CCM 2020/2025 agenda ya lishe imeingia kikamilifu kwani imekuwa kati ya vipaumbele vikubwa ya CCM.

Neema amesema kwa sababu watoto wanapokuwa na lishe duni hiyo ndio nguvu kazi ya kesho ili Taifa lolote likuwa lazima kuwepo na nguvu kazi thabiti ya kiuchumi

Amesisitiza kuwa aganda ya lishe imepata nafasi yake maalum kwenye ilani ya CCM ya Mwaka 2020/2025 kati ya malengo ni kushuha hali ya udumuvu hadi kufikia kiwango cha asilimia 24 ndani ya miaka mitano.
Mkurugenzi wa Shirika la Agri Thamani Foundation, Neema Lugangira akizungumza wakati wa semina hiyo
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Agri Thamani Foundation, Rehema Maro akizungumza wakati wa semina hiyo
KATIBU wa UWT Mkoa wa Tanga, Sophia Nkupe akizungumza wakati wa semina hiyo 
Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tanga (CCM) Husna Sekiboko
Sehemu ya washiriki mbalimbali kwenye semina hiyo
Sehemu ya washiriki kwenye semina hiyo wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi