Header Ads Widget

KMC YAANZA LIGI KIBABE, KAGERA YAPIGISHWA KWATA KAITABANa Damian Masyenene
LIGI Kuu Tanzania Bara baada ya kufunguliwa pazi lake jana, leo imeendelea tena kwa michezo miwili ya mapema, ambapo wana Kinondoni, timu ya KMC FC imeanza vyema ligi hiyo kwa ushindi mnono wa mabao 4 kwa 0 dhidi ya Mbeya City, mchezo uliopigwa kwenye dimba la Uhuru, Dar es Salaam.

Mabao ya KMC FC katika mchezo huo yalipachikwa dakika ya 21 kupitia kwa Israel Patrick, Hassan Kabunda dakika ya 39,  Abdul Hilary dakika ya 57 na Paul Peter dakika ya 74.

Kufuatia ushindi huo mnono, KMC sasa inaongoza ligi kwa alama tatu na faida ya mabao manne kibindoni, huku kichapo hicho kizito kikiifanya Mbeya City FC kuwa ya kwanza kukubali kufungwa mabao mengi, baada ya kuanza kwa msimu huu.

Katika mchezo mwingine uliopigwa leo, Wana Nkurukumbi, Kagera Sugar wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani Kaitaba wameshindwa kufurukuta mbele ya maafande wa JKT Tanzania, baada ya kukubali kipigo cha bao 1 kwa 0 lililofungwa na Adam Adam mnamo dakika ya 16.

Mchezo mwingine unatarajiwa kuchezwa saa moja usiku kati ya Azam FC dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es salaam.