Header Ads Widget

YANGA YAVUNJA BENCHI LA UFUNDI




Charles Mkwasa

KATIKA kile kinachoonekana ni kujipanga upya, Yanga imevunja benchi la ufundi kwa kuwaondoa kocha msaidizi, Charles Mkwasa, kocha wa makipa, Peter Mnyika, meneja Abeid Mziba na mtunza vifaa, Fred Mbuna.


Mkwasa ambaye amepumzika kazi, anaungana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Luc Eymael aliyefukuzwa baada ya kumaliza msimu huku wengine wakibadilishiwa majukumu. Yanga ipo katika kujipanga upya baada ya kumaliza msimu huu ikikosa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo.


Juzi ilitangaza kuwaacha wachezaji 14 kutokana na sababu ikiwemo kumaliza mikataba na wengine wakidaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu. Wachezaji walioachwa ni nahodha Papy Tshishimbi, David Molinga, Mrisho Ngasa, Jaffar Mohamed, Tariq Seif, Andrew Vicent na Mohamed Issa.

Wengine watakaositishiwa mikataba yao ni Ali Mtoni, Muharami Issa, Ali Ali, Patrick Sibomana, Eric Kabamba, Rafael Daud na Yikpe Gislain huku ikiwabakiza 17 pekee.
 Tayari mabingwa hao wa kihistoria wameanza kusajili wachezaji wapya na mpaka sasa imewasajili Waziri Junior kutoka Mbao, Yassin Mustapha kutoka Polisi Tanzania, Bakari Mwamnyeto kutoka Coastal Union na Zawadi Mauya kutoka Kagera Sugar kwa mkataba wa miaka miwili kila mmoja.

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Kamati ya ufundi wa klabu hiyo, Dominick Albinus alisema jana kuwa mabadiliko hayo yamelenga kuboresha utendaji kwenye timu ili kuleta tija msimu ujao.
“Kwenye timu ya wakubwa tutaendelea kuwa na kocha wa viungo Redoh Braden na mchua misuli, Fareed Cassim watakaoungana na kocha mpya na watendaji wengine watakaotangazwa hapo baadaye," alisema.