Header Ads Widget

TAKUKURU MANYARA YAMNASA HAKIMU MAGUGU KWA RUSHWA YA TSH 150,000


Na John Walter-Manyara.

Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Magugu Ndugu Adeltus Richard Rweyendera, amefikishwa mahakamani na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara kwa kosa la kuomba  na kupokea rushwa ya shilingi 150,000.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari, Kaimu mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara Isdory Kyando amesema mtuhumiwa huyo alipokea rushwa hiyo kutoka kwa wazazi na ndugu wa washtakiwa wanne ambao walikuwa wanashtakiwa kwenye kesi namba 242/2020 ikiwa ni kishawishi cha kuwasaidia na kuwaachia washtakiwa hao kwenye kesi tajwa ambayo alikuwa anaisikiliza.

Kyando amesema awali TAKUKURU Mkoa wa Manyara ilipokea taarifa kutoka kwa wasiri ikifafanua kuwa hakimu aliomba kiasi hicho cha fedha akiwataka wazazi na ndugu  wa washtakiwa hao wachangishane.

Amesema baada ya kupokea taarifa hiyo, walifanya uchunguzi wa kina na kubaini  ni kweli kesi tajwa ilikuwepo katika mahakama ya mwanzo Magugu na kwamba kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na hakimu Adeltus Richard Rweyendera
huku  kesi hiyo ikitajwa mara kadhaa bila kusikilizwa tangu ilipofunguliwa kwa mara ya kwanza tarehe 3/8/2020.

Uchunguzi wa Takukuru  ulibaini kuwa wananchi hao walikamatwa kwa tuhuma za uzururaji miongoni mwao wakiwa kwenye maeneo yao ya biashara.

Hata hivyo Takukuru walibaini kuwa  hakimu huyo aliwataka washtakiwa  wote  wanne  wachange kiasi hicho cha fedha.

Kyando amesema baada ya kujiridhisha na ukweli huo maafisa wa Taasisi hiyo,  waliandaa mtego wa rushwa na kufanikiwa kumkamata hakimu akiwa amepokea kiasi cha shilingi 150,000/ fedha ambazo aliziweka kwenye droo ya meza yake mara baada ya kuzipokea.

Aidha TAKUKURU imemuunganisha kwenye mashtaka ndugu Issaya Kiluma ambaye alikubaliana hakimu huyo kutoa rushwa hiyo akichangia jumla ya shilingi 40,000 ikiwa ni sehemu ya shilingi 150,000/= ambazo hakimu alikamatwa nazo.

Kyando ameongeza kuwa Bwana Kiluma alikuwa  miongoni mwa ndugu wa washtakiwa ambaye alikubaliana na hakimu kutoa kiasi hicho cha fedha pasipo kutoa taarifa TAKUKURU.

Amesema kuwa mwananchi huyo ataunganishwa kwenye mashtaka ya kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kutoa rushwa ambapob  kosa hilo lina  uzito sawa na kosa la kupokea rushwa.

Kwa upande mwingine Takukuru imetoa  wito kwa wananchi wa mkoa wa Manyara na watanzania kwa ujumla kuacha kuwashawishi na kutoa rushwa kwa watumishi wa Idara ya mahakama na kwingineko kokote na pale wanapoombwa rushwa wasisite kutoa taarifa katika ofisi za TAKUKURU zilizopo kote nchini.

Aidha Kyando, amewataka   watumishi wa idara ya mahakama ambayo ni wadau wakubwa wa mapambano dhidi ya ya rushwa na ambao wanafanya kazi muhimu sana ya kusimamia haki za watanzania kuhakikisha kuwa wanawasimamia ipasavyo watumishi wachache ambao sio waadilifu na kuwachukulia hatua stahiki pale inapothibitika kuwa wamejihusisha na vitendo hivyo.