Header Ads Widget

MTAFITI AWEKA WAZI SABABU ZA MAGONJWA YA WANYAMA YANAVYOKWENDA KWA BINADAMU


MTAFITI kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) Dk.Iddi Lipende ametaja sababu kadhaa zinazochochea magonjwa ya mambukizi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na hivyo kuleta taharuki kubwa kwa jamii akitolea mfano janga la Corona.

Dk.Lipende ametoa sababu hizo alipokuwa akitoa mada yake kwenye semina iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania(JET) ikiwa ni mkakati wake wa kuendelea kuwajengea uwezo waandishi wa habari nchini katika kuandika habari zinazohusu uhifadhi wa mazingira na wanyamapori kwa ujumla.

JET imeandaa semina hiyo chini ya ufadhili wa Mradi wa kulinda mazingira na kukuza uhifadhi na utalii nchini Tanzania ujulikanao kwa kifupi kama mradi wa PROTECT (Promoting Tanzania’s Environment, Conservation, and Tourism).

"Kwa ujumla tunaweza kueleza haya magonjwa mtambuka yanaweza kutokea katika sehemu mbili.Moja ni kwamba magonjwa haya yanapohama kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu inatokea mara chache sana.

"Lakini unapongia kwa binadamu tena unaanzisha kuhamisha kutoka kwa mwanadamu kwenda kwa mwanadamu bila mnyama kuwepo, na hii ndio tumeona imetokea kwenye magonjwa kama Ebola, Mafua ya ndege na Corona na magonjwa mengine ya aina hiyo.

"Pili kuna uwepo wa magonjwa yaani ugonjwa unatoka kwa mnyamapori kwenda kwa binadamu lakini unapofika kwa binadamu ni mra chache sana kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu.
"Kwamba huu ugonjwa lazima uupate kwa wanyamapori au mnyama , mfano ni pale tunapopata ugonjwa kama kichaa cha Mbwa, kichaa cha mbwa unakipata pale ambapo unaumwa na mbwa mweye kichaaa.

"Ni mara chache sana ana uwezo wa kusababisha huu ugonjwa kwa watu wanaomzunguka labda iwe au kwa kuwamua au wakati anatibiwa majeraha.Na kuna magonjwa mengine ambayo unaweza kuyapata kwa panya lakini huwezi kusambaza kwa jirani yako,"amesema.

Ametaja sababu nyingine ya kuhamisha magonjwa ya wanyama kwenda kwa binadamu ni kwenye masoko ya wanyamapori."Haya ni maeneo maalumu yanatengwa kwa ajili ya kuuza nyama au bidhaa nyingine zinatokana na wanyamapori.Pia kuna hii biashara ndogo ya wanayamapori kwa ajili ya kufuga nyumbani, sasa kutokana na kukua kiuchumi watu wanatamani kufuga hata wanyama ambao hata kwa asili tu hatuvifugi.

"Mtu anataka kufuga mjusi, kenge, mamba, mtoto wa sokwe na aina nyingine za wanyama, haya ndio mambo yanayosababisha kuwepo wa shida hizi za magonjwa ambazo tunaziona.Haya masoko tunayoyaona wakati mwingine yanakuwa masoko ya halali  na mengine haramu,"amesema Dk.Lipende.

Amefafanua katika masoko haramu yanayofanyika ni pamoja na kuongezewa na vitu halali ambavyo vinaingia ndani yake na kwamba kwa Afrika au Tanzania shida kubwa ya wanyamapori katka soko wanakimbilia kwenye kula na hawana shida sana ya kufuga.

"Lakini hii ya nyama pori tunaingilia tangu ilipoanzia ,sisi ulaji wetu wa wanyama umeanzia mpaka kwenye panya, wengine wameenda mbali zaidi mpaka wanyama wakubwa kama Pundamilia, Nyati, Kima na Sokwe na hapa tunaangalia uwepo wa ukaribu wa vinasaba kati ya wanyamapori, wanyama wa nyumbani na binadamu upo mkubwa sana.

"Kwa mfano ni Sokwe ambaye tumekaribiana naye kwa karibu asilimia 98.9 , kwa vinasaba, kwa hiyo ni rahisi sana kwa mdudu kuingia kwa binadamu na wakati mwingine tunapata ukaribu wa damu ya mnyama kuingia kwa binadamu.

"Na hii inafanywa sana kwa wawindaji wanapokwenda kuwinda, wanamchoma mikuki na kumtoa majereha yanayotoa damu nyingi na hata wakati anapoandaliwa ile damu yake inaweza kuingia kwa binadamu na kusababisha magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu,"amesema.

Hata hivyo ameeleza sababu zinazosababisha watu kupenda kula nyamapori ni kwamba wanaona ni njia ya kubadilisha chakula.Pia kukua kwa jadi na tamaduni za watu ya watu na hivyo kuamini nyamapori ndio chakula kizuri sana au kinaonekana cha kifahari. "Kula nyama ya wanyamapori inasababisha kwa ukaribu sana kuhamisha magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu .Wengi wetu tunapenda sana nyama za porini.

"Hakuna anayeuliza nyama ya porini inapatikanaje?Ni ile inayokwenda kuwindwa usiku , zinabebwa begani na kuletwa kijijini watu wanauiziwa  na kisha wanakula tena nyama ambayo haijapimwa na hakuna anayejua kama mnyama ambaye amewindwa ni sehemu ya wanyama wenye udhaifu.
" Pili inaonekana sasa hivi ni rahisi sana kupata nyama ya porini kwasababu kukamata mnyama mjanja kama  swala imekuwa jambo la kawaida kutokana na kukua kwa teknolojia.Uwindaji umekuwa wa haraka sana.

"Mtu anaweza kuwinda nyama usiku na bado ikiwa inaendelea kuvuja damu nyingi inaweza kufika Mwanza kabla hata haijakauka.Hii inatokana na urahisi wa usafirishaji kutokana na kuimarika kwa miundombinu ya barabara na usafirishaji kwa ujumla,"amesema.

Hivyo amesema kwa mazingira ya aina hiyo sasa uwepo wa magonjwa unaongezeka sana kutokana na muingiliano uliopo."Tumeona jinsi ambavyo masoko yetu ya wanyamapori yanavyoweza kutuletea magonjwa. 

"Haya mahusiano ya ugonjwa kutoka kwa wanyamapori kwenda kwa binadamu yanaweza ikatokea moja kwa moja kwasababu ya kula mchuzi au kula nyama isiyopikwa vizuri ambayo damu ya mnyama haijakauka ikaingia kwa binadamu na kusababisha ugonjwa,"amesema Dk.Lipende.

Hata hivyo amesema sababu nyingine ni ya kimazingira ambapo amefafanua "Kama tunavyoona kuna watu wanaingia kulima kwenye maeneo yanayotumiwa na wanyamapori , wanaingia na kukaa kule, wanachota maji kwenye kisima ambacho usiku Nyati, Nyumbu, Tembo,Swala, Paka au aina nyingine ya mnyama aliingia kunywa maji.

"Muingiliano huo wa kimazingira unachangia kuhamisha magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu,"amesisitiza Dk.Lipende na kuongeza kwa hali hiyo ndio maana kumekuwepo na magonjwa mengi ambayo binadamu wanayo lakini msingi wake wameyapata kwa wanyama.

Amesema kama ilivyoonekana kwenye Corona awali haukuwa wa ugonjwa wa binadamu, ulikuwa ugonjwa ambao unaoekana kuwa karibu sana na Popo na Panya."Hao ni wanyama ambao tumeona hatuwajali lakini ni wanyama hatarishi.

"Kwani wengi wameonekana wanabeba wadudu ambao tunakaribiana nao sana, na hivyo tunavyokuwa nao karibu tunajiweka kwenye hatari ya kuambikizwa magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu,"amesema Dk.Lipende.