Header Ads Widget

WANACHAMA 10 CCM WATIA NIA UBUNGE SHINYANGA MJINI

Stephen Masele
Na Damian Masyenene –Shinyanga Press Club Blog
ZIKIWA zimebaki siku tano kufunguliwa kwa milango kwa watia nia wa nafasi za Ubunge na udiwani ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanza kuchukua fomu za kugombea, tayari imebainika kuwa wanachama 10 wameonesha nia ya kugombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini.
Watu hao 10 ni kutoka ndani ya chama hicho ambayo wanahitaji kuleta ushindani kwa Stephen Masele ambaye amekuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 10 sasa.
Akizungumza katika mkutano wake na Waandishi wa habari ofisi kwake leo Julai 9, 2020, Katibu  wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Saidi Bwanga amesema kuwa zoezi la uchukuaji fomu litaanza Julai 14 na kufungwa Julai 17, mwaka huu saa 10 jioni.
Bwanga amewataja waliotia nia kuwa ni Stephen Masele (aliyekuwa mbunge), Bandora Mirambo, Wilbert Masanja,  Severine Kilulya, Erasto Kwilasa na Jonathan Manyama.
Wengine ni Dotto Joshua na wanawake watatu ambao ni Lydia Pius, Mary Izengo na Eunice Jackson.
Bwanga amesistiza kwamba CCM imejipanga ili kupata viongozi bora wasiotokana na shinikizo la fedha, huku akiishukuru Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani hapa kwa kazi kubwa wanayoifanya kudhibiti vitendo hivyo kwa watia nia.
“Tunawaomba Takukuru waendelee kuongeza nguvu kwa sababu hata sisi (CCM) tunakereka na tabia hizi na mara kwa mara tumekuwa tukikemea ndani ya chama kwa kuzungumza na viongozi, wagombea na wanachama,” alisema.