Header Ads Widget

VIONGOZI 12 WA CCM SHINYANGA MJINI WASIMAMISHWA UONGOZI KWA TUHUMA ZA RUSHWA

Katibu wa Siasa na Uenezi Wilaya ya Shinyanga Mjini, Saidi Bwanga
Na Damian Masyenene –Shinyanga Press Club Blog
KIKAO cha Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini mkoani Shinyanga kimewasimamisha nyadhifa zao zote viongozi 12 wa Kata ya Ngokolo kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma za rushwa zinazowakabili.
Uamuzi huo umetangazwa leo Julai 9, 2020 na Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Shinyanga, Saidi Bwanga katika mkutano wake na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo amesema kuwa hatua hiyo ni kutekeleza kwa vitendo nia ya chama hicho kupata viongozi wasiotokana na shinikizo la pesa pamoja na kukomesha rushwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Bwanga alisema uamuzi huo ni matokeo ya kikao cha kamati ya siasa kilichoketi Julai 8, mwaka huu na kuja na mapendekezo hayo ya kuwasimamisha uongozi hadi pale majibu kutoka vyombo vya dola yatakapotoka ndiyo itaamuliwa vingine aidha kurudishiwa nafasi zao ama kuondolewa jumla.
”Chama chetu kimepokea taarifa mbalimbali kutoka vyombo vya dola kwa baadhi ya wanachama wetu kwenda kinyume na maagizo ya chama kwa kujihusisha na rushwa, hivyo tumeamua kukaa na kuja na maamuzi hayo ya kuwasimamisha mpaka pale uchunguzi kwenye vyombo vya dola utakapokamilika.
“Mara kwa mara tumekuwa tukikemea ndani ya chama kwa kuzungumza na viongozi, wagombea na wanachama ili kudhibiti vitendo hivi, kwa sasa tumewasimamisha nafasi zao za Uongozi wakibainika wana makosa wanapata adhabu lakini ikionekana tofauti watarudishiwa nyadhifa zao,” alisema.
Waliosimamishwa Uongozi kwa tuhuma za rushwa katika kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga ni Helda Malsaba ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) katika kata hiyo, Pendo Mhapa (Katibu wa UWT Ngokolo), Zulfa Hassani (Mwenezi wa kata hiyo), Jackline Isalo (Mjumbe wa Kamati ya utekelezaji ya UWT wilaya) na Asha Mwandu ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa na mjumbe wa kamati ya utekelezaji CCM mkoa.
Wengine ni Elizabeth Hange (Katibu wa UWT tawi la Ngokolo), Moshi Ndugulile (Mjumbe wa kamati ya utekelezaji UWT wilaya), Tabu Shabani (Katibu wa UWT tawi la Ngokolo), Tabu Said (Kamati ya utekelezaji wazazi), Happy Chikala (katibu UWT tawi la Mwadui), Elizabeth Buzwizwi (Katibu UWT tawi) na Elizabeth Benjamin ambaye ni Mwenyekiti wa UWT tawi la Mwadui.