Header Ads Widget

NGOs ZATAKIWA KUUNGA MKONO JITIHADA ZA SERIKALI MIRADI YA MAENDELEO



Dk. John Jingu

Na Mwandishi Wetu -Tanga

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu ameyataka mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kuunga mkono jitihada za Serikali za kuendeleza miradi ya maendeleo badala ya kubaki na dhana ya kukosoa kila jambo.

Dkt. Jingu ameyasema hayo wakati akikagua ujenzi wa barabara iliyojengwa na wananchi wa kijiji cha Wangwi wilayani Lushoto kwa kushirikiana na shirika la New Hope Community Development pamoja na Serikali kupitia Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mabughai na Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto.

“NGOs ni wadau wa maendeleo na wanapenda kujiita wanaharakati, harakai nzuri ni kama hizi za kubainisha matatizo yaliyopo kwenye jamii na kuhamasisha kama walivyofanya New Hope, uanaharakati siyo kuonesha tu mapungufu waliyonayo wengine” amesema.

Amezitaka NGOs nyingine kuiga mfano huo wa kushirikiana na Serikali kutatua changamoto zilizopo.

Mkurugenzi wa Shirika la New Hope, Baraka Chambua, amesema barabara hiyo yenye urefu wa takribani kilomita 20 imejengwa na wananchi wenyewe kutokana na uhamasishaji uliolenga kuwasaidia wananchi kusafirisha mazao na wao wenyewe.

“Asilimia kubwa ya kazi hii imefanywa na wananchi, ikikamilika itasaidia mazao yao yasiharibike kwa kuyasafirisha hadi kijiji jirani kwa urahisi.

 "Kazi kubwa iliyofanywa na shirika ni kuwapa moyo na kushirikiana na Chuo cha Mabughai kuhakikisha wanakijiji wanapata mafunzo maalum yatakayowasaidia katika ujenzi wa barabara hii,” amesema Chambua.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Joyce Israel amesema Halmashauri imeshirikiana vema na wanakijiji hao na tayari mawasiliano yameshafanyika na Wakala wa Barabara Vijijini TARURA kuiweka barabara hiyo kwenye mipango yake ili waweze kuiendeleza.

Baadhi ya wa wanakijiji wameishukuru Serikali pamoja na shirika hilo kwa kuwahamasisha hatimaye wameweza kuwa na barabara inayosaidia kusafirisha mizigo na wao wenyewe kwani mwanzoni hawakuwa na barabara.