Header Ads Widget

TAKUKURU TABORA YAOKOA SH. MILIONI 74, ZIMO ZA WASTAAFU WALIOBAMBIKIWA RIBA KUBWA

 
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Tabora, imeokoa zaidi ya Sh milioni 74 katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye miradi ya maendeleo, vyama vya ushirika na mikopo umiza na kuzirejesha kwa wenyewe.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tabora, Musa Chaulo, alisema kati ya fedha zilizookolewa Sh 24,640,000 iliyotolewa bila kufuata utaratibu ambazo zimerejeshwa kwa wenyewe.

Alisema taasisi hiyo ilifanya uchunguzi na kubaini uonevu na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za ukopeshaji kwani wakopesha waliwataka wakopaji ambao ni wastaafu riba ya asilimia 500 ndani ya miezi minne.

Alisema pia kupitia dawati la uzuiaji rushwa, taasisi hiyo imefuatilia mradi wa ujenzi wa majengo na ukarabati wa miundombiny ya Shule ya Sekondari ya Milambo unaogharimu Sh 522,072,250.

Alisema walipokea malalamiko 54 ambayo kati yake 29 yalikuwa ya viashiria vya rushwa, watoa taarifa 13 walipewa ushauri kulingana na malamlko yao na 12 yalihamishiwa idara nyingine kwa ufuatiliaji zaidi.

Alisema wakati wa kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais utakaofanyika Oktoba mwaka huu, Takukuru mkoa imeweka mkazo wa kuelimisha jamii ili kuhakikisha wanapatikana viongozi wenye maadili.
 
 Kufuatia hilo Chaulo aliwataka wananchi na wanasiasa kufuata taratibu na sheria za nchi na kuhakikisha hawajihusishi na vitendo vya rushwa na yeyeto atakaye bainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Aliwakumbusha wananchi kutokubali kurubuniwa na wagombea na kupewa rushwa kwani athari zake ni kubwa.