Header Ads Widget

JPM: SIJAMTUMA YEYOTE AKACHUKUE FOMU YA UBUNGE, WAGOMBEA CCM WAFIKA 8,205Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli

Na Damian Masyenene -Shinyanga Press Club Blog
KUFUATIA uwepo wa fununu na maneno lukuki juu ya makada mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaojitokeza majimboni kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama hicho kuwania ubunge, kuwa wametumwa na Rais na wana uhakika wa kushinda, leo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. John Magufuli amezima tetesi hizo kwa kueleza kuwa hajamtuma mwana CCM yeyote kuchukua fomu.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Julai 16, 2020 Ikulu ya Chamwino, Dodoma wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi na makatibu tawala wapya, huku akiwapongeza makada wote wa chama hicho waliojitokeza kuchukua fomu hadi sasa.

JPM amesema hajamtuma mwanachama yeyote awe Mkuu wa Mkoa, wilaya, Mkurugenzi ama mwanasiasa yeyote kuchukua fomu, na wala hakuna aliyetumwa na Waziri Mkuu, Makamu wa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi, hivyo akawataka wanachama wa CCM kuwahukumu na kuwapima wagombea hao kwa usawa kwa manufaa ya chama hicho ili wapate mtu sahihi.

"Nawapongeza wale wote waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali, niwaombe tu wakazingatie nidhamu na maadili ya chama chetu,
niwathibitishie tu kwamba hakuna mtu yeyote aliyetumwa na mimi, waziri mkuu, makamu wa rais, kama kuna watu wanazungumza kwamba mimi nimewatuma ni uongo.

"Wana CCM nyinyi wapimeni wagombea kulingana na nyinyi mnavyowaona wanafaa, wote wako sawa wapimeni kisawasawa," amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amesema hadi kufikia leo mchana, Jumla ya Wanachama 8205 wamechukua fomu ndani ya CCM, huku mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa kufikisha wagombea 829, Arusha 320, Kagera 328 na Kilimanjaro 82, huku Viti Maalum wakijitokeza wagombea  1,539 na wawakilishi 133.