Header Ads Widget

WAZIRI JAFO AMSHANGAA DC SUMBAWANGA KUZIDISHA LIKIZO, ATAKA KUMSHTAKI KWA RAIS


Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Dk. Halfan Haule

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jaffo amemjia juu Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk. Halfan Haule kwa kile alichodai kuwa ni mtovu wa nidhamu baada ya kuomba likizo ya siku 14 na akaamua kukaa zaidi ya mwezi mmoja bila taarifa.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Sumbawanga amesema kuwa, kitendo alichokifanya mkuu huyo wa wilaya kinaonesha pia utovu wa nidhamu wa watumishi katika wilaya yake pia.

Amesema kuwa, pamoja na kitendo hicho ofisi ya Tamisemi ilimuandikia barua ili kumpa nafasi ajieleze kwa nini alifanya hivyo, lakini bado amekaa kimya kana kwamba hakufanya kosa lolote.

“Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga aliomba likizo ya siku 14, lakini akakaa zaidi ya mwezi mmoja bila kutoa taarifa na hata ofisi ya Tamisemi ilipo mwandikia barua hajajibu mpaka leo, na bado katika wilaya yake ndiko kuna matumizi mabaya ya fedha za serikali na hakuna hatua zilizochukuliwa.

“Nitakwenda kumwambia Rais John Magufuli maana yeye ndio mamlaka ya uteuzi achukue hatua katika hili, hatuwezi kuendelea kuwafumbia macho viongozi wa namna hii, tunataka maendeleo kwa kasi kubwa na viongozi ndio wanapaswa kuwa mfano,” amesema Waziri Jafo.

Aidha, Waziri huyo wa Tamisemi alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo kusimamia nidhamu kwa baadhi ya viongozi wa mkoa huo,licha ya kuwa yeye anafanya vizuri, lakini anakwamishwa na viongozi hao wenye kiburi na watovu wa nidhamu akiwemo mkuu huyo wa wilaya.

Chanzo: Times Majira.com


Post a Comment

0 Comments