Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (wa pili kulia) akizungumza na wanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya sekondari Kishapu alipofanya ziara kujionea utayari wa shule hiyo kupokea wanafunzi waliorejea kuanza masomo.
Na Catherine Ngowi - Kishapu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack amewataka viongozi
wa shule za sekondari hususan zilizopokea wanafunzi wa kidato cha sita
walioanza masomo Juni mosi, mwaka huu, kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuweka
mazingira mazuri ambayo yatawafanya wasibanane mabwenini kwani ugonjwa wa COVID-19
bado upo.
Mkuu huyo wa mkoa amesisitiza pia wanafunzi kuendelea
kufundishwa njia bora za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo ikiwemo kunawa mikono
kwa usahihi na kuweka miundombinu yote inayohitajika kwa ajili ya kuchukua
tahadhari, huku maofisa elimu nao wakitakiwa kushirikiana na walimu katika
kipindi hiki.
RC Telack ametoa maagizo hayo leo Juni 2, 2020 wilayani
Kishapu mkoani hapa baada ya kuzitembelea na kuzikagua shule za sekondari
Shinyanga na Kishapu zenye wanafunzi wa kidato cha tano na sita alipokuwa akikagua
hali ya maandalizi kwa shule hizo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 unaoambukizwa na
virusi vya Corona.
“Nia yetu ni kuhakikisha kuwa mnakuwa salama, wanafunzi wakipata
maambukizi na nyie walimu mtapata, jikingeni kwa sababu Corona ipo. Pia katika
mabweni yao ya kulala hakikisheni wanapata nafasi za kutosha wasibanane. Nanyi
Maafisa elimu shirikianeni na walimu katika kipindi hiki cha Corona kutatua
changamoto katika shule hizi,” amesema RC Telack.
Aidha Mkuu wa Mkoa amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii kwa
kushirikiana pamoja ili kujiandaa vyema na mitihani ijayo, huku akiagiza uongozi
wa shule hizo kuhakikisha wanafunzi wanakula chakula bora na kwa wakati ili kufanya
vyema katika masomo yao.
“Someni kwa pamoja kwa sababu tunataka wote mtoke mkiwa mmefaulu
hivyo mshirikiane na msaidiane kwenye masomo angalau kila mtu aweze kufaulu
kwenda chuo kikuu. Sasa hivi acheni kulala, tumieni huu muda uliobaki vizuri
kwa sababu hatutaki daraja la tatu wala sifuri, nataka kuona kila mtu akipata daraja
la kwanza,” amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Kulingana na ratiba iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia chini ya Waziri mwenye dhamana Profesa Joyce Ndalichako, wanafunzi wa kidato cha sita wanatarajia
kuanza mtihami wa taifa Juni 29, 2020.