Header Ads Widget

MTENDAJI MKUU WA ZAMANI MSD MBARONI KWA RUSHWA, SIKU 30 BAADA YA KUTUMBULIWA NA JPM


Bw. Laurean Bwanakunu

Na Mwandishi Wetu - Shinyanga Press Club blog
Ikiwa ni takribani siku 30 baada ya uteuzi wake kutenguliwa mnamo Mei 3, mwaka huu, aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Bohari ya Madawa nchini (MSD), Laurean Bwanakunu anashikiliwa kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma za rushwa zinazomkabili. 

Bwanakunu anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) makao makuu kuanzia leo Juni 2, 2020 pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Lojistiki wa MSD, Byekwaso Tabura. 

Watuhumiwa wote wawili wapo mahabusu katika ofisi za taasisi hiyo zilizopo Upanga jijini Dar es Salaam kuanzia leo Juni 2, 2020 kupisha uchunguzi. 

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Juni 2, 2020 na Afisa Uhusiano wa Takukuru Makao Makuu, Doreen Kapwani, watuhumiwa hao wanakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara kinyume na Sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Namba 11 ya mwaka 2007. 

Ikumbukwe kuwa Mei 3, mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli alitengua uteuzi wa mkurugenzi huyo (Bwanakunu) na kumteua Brigedia Jenerali Dkt. Gabriel Mhidize kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa MSD. 

Ambapo uteuzi huo ulifuata baada ya Rais Dk. John Magufuli kueleza kuwa sampuli kadhaa ambazo hazikuwa za binadamu zilitumwa katika maabara ya taifa ili kupima ubora na usahihi wa majibu ya mashine hizo katika vipimo vya ugonjwa wa COVID-19 na kuleta majibu yaliyoacha maswali mengi. 

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo Mei 3, 2020 wilayani Chato wakati akimuapisha Waziri mteule wa Sheria na Katiba, Mwigulu Nchemba. 

Bwanakunu aliiongoza MSD tangu mwaka 2015 baada ya kuteuliwa na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete.