Header Ads Widget

SERIKALI YATANGAZA MIFUMO MITATU UUZWAJI WA KAHAWA, BODI YAPEWA RUNGU



Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza mikakati ya serikali kwenye zao la Kahawa wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya Kahawa Wilayani Mbozi Mkoani Songwe uliofanyika katika ukumbi wa kanisa la Moravian Sala-Ichenjezya leo Juni 9, 2020.

Na Mathias Canal - Wizara ya Kilimo, Songwe

Ili kukabiliana na changamoto ya uuzaji wa mazao mbalimbali ya wakulima nchini katika kipindi hiki cha Ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona serikali imetangaza na mifumo mitatu ya uuzaji wa Kahawa.

Mifumo hiyo ni uuzaji wa kahawa kwa soko la moja kwa moja (Direct Selling), Mfumo wa kuuza kupitia minada ambapo vyama vya ushirika vitakusanya mazao kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani na mfumo wa tatu ni wakulima kuingia makubaliano na wamiliki wa viwanda vya ndani ya nchi vya uchakataji wa kahawa ili kuwauzia kahawa yao. 


Serikali imewataka wakulima kutumia fursa hiyo ya uuzaji wa kahawa kwenye maeneo watakayoona kuna wanunuzi wenye bei nzuri lakini wauzaji hao wasiende moja kwa moja kwa wakulima badala yake wanunue kahawa kupitia kwenye vyama vya Ushirika.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (Mb) leo  Juni 9, 2020 wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya Kahawa wilaya ya Mbozi mkoani Songwe uliofanyika katika ukumbi wa kanisa la Moravian Sala-Ichenjezya. 
Waziri Hasunga ameikumbusha Bodi ya Kahawa Tanzania kuwa ndiyo yenye jukumu la kusimamia sekta ya Kahawa, hivyo inapaswa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu za nchi. Ambapo amewataka maafisa Ushirika kutekeleza wajibu wao sio kupinga maelekezo ya Bodi hiyo yanayotolewa kwa niaba ya serikali. 


Amesema kuwa serikali haiwezi kuzuia wanunuzi binafsi kwani biashara ya mazao na bidhaa zingine ni muhimu kuzingatia taratibu, kanuni na sheria za nchi hivyo hivyo ushindani ni muhimu ili kuimarisha bei ya mazao ya wakulima.

Waziri Hasunga amesema kuwa serikali inazo taarifa za kutosha juu ya Afisa Ushirika wa Wilaya ya Mbozi, Fredy Katoto kuihujumu serikali kwa kutotekeleza maagizo yanayotolewa na viongozi mbalimbali hivyo serikali itamchukulia hatua kali za kisheria mtumishi huyo kwani anawapotosha wakulima.

“Mtumishi wa Umma ambaye umeajiriwa unawadanganya wakulima, na wewe ndiye umekuwa tatizo kwenye kilimo chetu mnakaa huko mnapanga namna ya kulipa lakini hamlipi kwa maelekezo ya serikali taarifa tunazo, Kuna wakulima mpaka sasa hivi hawajalipwa fedha zao kwa sababu ya Katoto huyu nitamshughulikia,” Alikaririwa Waziri Hasunga.

Katika usimamizi madhubuti wa sekta ya ushirika nchini, Waziri wa Kilimo Mhe Hasunga amesema kuwa ili kudhibiti wizi na ubadhilifu kwenye vyama vya ushirika unaojitokeza mara kwa mara serikali imeamua kuja na mkakati wa kuwaajiri mameneja wa vyama hivyo ili kusimamia na kudhibiti mali na fedha zote za wakulima. 


Akizungumza kwa niaba ya wanunuzi binafsi wa kahawa, Tikson Nzuda amesema kuwa wanunuzi hao wana fedha za kutosha za kununua kahawa yote ya wakulima hivyo wameiomba serikali kuwapatia leseni haraka iwezekanavyo ili waingie sokoni. 


Ameongeza kuwa wanunuzi binafsi tayari wamekopa fedha kwenye Taasisi mbalimbali za kifedha zikiwemo benki lakini mpaka sasa hawajapewa kibali jambo ambalo ni hatari kwao katika mikopo hiyo.

Sehemu ya wadau wa sekta ya Kahawa wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (Mb) kwenye ukumbi wa kanisa la Moravian Sala-Ichenjezya leo  Juni 9, 2020.

Sehemu ya wadau wa sekta ya Kahawa wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (Mb) kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya Kahawa wilayani Mbozi mkoani Songwe   Juni 9, 2020. 
Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo