Header Ads Widget

CHADEMA WALITAKA JESHI LA POLISI NCHINI KUPANUA WIGO WA UCHUNGUZI TUKIO LA KUSHAMBULIWA MBOWE


Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelitaka Jeshi la Polisi nchini kupanua wigo wa uchunguzi wa tukio la kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe usiku wa kuamkia mapema leo jijini Dodoma.
Kimesema uchunguzi huo utakaofanywa na Jeshi la Polisi unapaswa kutosita kuchunguza mazingira ya kisiasa ya tukio hilo yaliyozunguka na kauli zilizotolewa awali kabla ya kufanyika kwa shambulio hilo.
Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,ameshambuliwa usiku wa kuamkia jana wakati akirejea nyumbani kwake Area D jijini Dodoma.
Akizungumza leo waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, amesema Mbowe anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya DCMCT Ntyuka jijini humo Dodoma na kwamba chama kimefikia uamuzi wa kadri ya ushauri wa madaktari watakaoendelea kuwapa watafanya utaratibu wa kumsafirisha kuja Jijini Dar es Salaam ili kuweza kupatiwa matibabu zaidi.
Amesema taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi leo  imesema kuwa tukio hili ni la kawaida na kwamba lisihusishwe na na masuala ya kisiasa.
Mnyika amesema kwa sababu jeshi la polisi limesema linafanyia uchunguzi, hivyo halipaswi kufunga uchunguzi na kuliita tukio hilo ni la kawaida.
“Natoa wito kwa Jeshi la Polisi na vyombo vya ulinzi na usalama vilichunguze jambo hili kwa mapana na mawanda yake yote ili waliohusika na tukio hili wafahamike kwa haraka na hatua za haraka ziweze kuchukuliwa dhidi yao,”amesema Mnyika.