Header Ads Widget

RATIBA VPL HADHARANI, MWADUI VS YANGA JUNI 13 KAMBARAGE
  Kikosi cha Mwadui FC
 
Na Damian Masyenene

Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) leo Juni mosi, 2020 imeweka wazi ratiba ya Ligi Kuu (VPL) itakayoanza Juni 13 mwaka huu, ambapo siku hiyo itachezwa michezo miwili pekee, ambapo mchezo utakaovuta hisia za wapenda soka wengi nchini ni ule utakaopigwa kwenye dimba la CCM Kambarage, mjini Shinyanga wenyeji Mwadui FC wakiwakaribisha Wana Jangwani, Yanga SC.

Mchezo huo wa mzunguko wa 17 ni kiporo na utachezwa saa 10 jioni uwanjani hapo, huku Mwadui wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuwafunga vinara wa ligi hiyo, Simba SC kwa bao 1-0 uwanjani hapo, mwishoni mwa mwaka jana.

Mchezo mwingine utakaopigwa Juni 13, mwaka huu ni baina ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga itakayowaalika kwenye dimba la Mkwakwani vijana wa Namungo FC kutoka mkoani Lindi.

Michezo mingine itaendelea Juni 14, 2020 pale ambapo Wekundu wa Msimbazi Simba SC watakapoikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku katika dimba la kisasa la Azam Complex Chamazi, Matajiri wa Azam FC watakuwa wenyeji wa Mbao FC ya Mwanza majira ya saa 1 usiku.

Ligi hiyo itaendelea Juni 17, mwaka huu kwa mchezo mmoja, ambapo JKT Tanzania ambayo imehamia jijini Dodoma itawakaribisha Mabingwa wa Kihistoria, Yanga SC kwenye uwanja wa Jamhuri majira ya saa 10 jioni.


TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807