Waziri wa Kilimo Mhe Japhet
Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akitangaza msimamo wa serikali kuhusu
Mazao yatakayouzwa kwa mfumo wa Stakabadhi Ghalani ofisini kwake Jijini Dodoma.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imetangaza rasmi mazao ya kuanzia
yatakayouzwa kupitia mfumo maalumu wa uuzaji wa mazao wa Stakabadhi ghalani.
Mazao hayo ni pamoja na zao la Korosho ambalo
limekuwa na mafanikio makubwa kupitia mfumo huo, mazao mengine ni Ufuta ambao
utauzwa kwa mfumo huo katika baadhi ya maeneo nchini.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)
ametangaza msimamo huo wa serikali wakati akizungumza ofisini kwake Jijini
Dodoma juzi tarehe 30 Mei 2020 huku akiyataja mazao mengine yaliyoingizwa
katika mfumo huo kuwa ni pamoja na Choroko, Pamba, Dengu, pamoja na Kahawa
itakayotumia mfumo huo kwa baadhi ya maeneo.
Waziri Hasunga amesema kuwa mfumo huo tangu
umeanza kutekelezwa umekuwa na faida kubwa hususani katika mikoa ya kusini
kupitia zao la korosho lakini umeleta changamoto kubwa katika maeneo ambayo
misingi ya kuanzishwa kwa mfumo huo haijatimizwa.
Amesema kuwa ili mfumo wa Stakabadhi ghalani
uweze kufanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa ni lazima kuwa na vyama vya
Ushirika vya mazao vilivyoanzishwa na wananchi wenyewe katika eneo husika.
Ameeleza kuwa lengo la kuwa na vyama hivyo ni
kufanya kazi ya kukusanya mazao na kuyapeleka kwenye ghala kuu ambalo
limesajiliwa na kuwa na viwango vinavyotakiwa.
Jambo jingine ni lazima kuwepo na muendesha
ghala mwenye leseni anayetambuliwa na Bodi ya Maghala na lazima elimu ya
kutosha itolewe kwa wananchi ya namna ya kutumia mfumo huo na ushiriki wao
katika kufuatilia minada itakavyokwenda.
Amesisitiza kuwa ili mfumo huo uweze kufanya
kazi vizuri wanunuzi lazima wawepo, Mfumo utangazwe na kuuzwa hadharani
kadhalika kuwe na mzigo wa kutosha pamoja na ubora wa uhifadhi ili kuwavutia
wanunuzi.
Ameeleza kuwa sio mazao yote yanaweza kutumika
katika mfumo wa stakabadhi ghalani ni baadhi ya mazao kulingana na uwezo wake
wa kutunzwa na kukaa muda mrefu bila kuharibika. Hivyo kwa mazao ya mboga na
matunda haiwezi kuwa jambo jepesi kuzitunza muda mrefu hivyo sio rahisi kuingia
katika mfumo wa stakabadhi ghalani.
“Ukichukua mazao kama karanga ukaweka kwenye
mfumo huu, unaweza ukahifadhi lakini tatizo la karanga zinaweza zisiwe na
unyevu unaokubalika hivyo kuna hatari ya kusababisha Sumu kuvu.
Waziri Hasunga amesema kuwa lengo la kuanzishwa
kwa mfumo wa Stakabadhi ghalani ilikuwa ni kulinda maslahi ya wakulima kwani
mazao hukusanywa pamoja, kuwekwa kwenye madaraja kisha kupanga bei kwa pamoja
hivyo kuuza kwa bei nzuri.
Mfumo huo unamuwezesha mkulima kupata mkopo
popote baada ya kuwa na risiti ya stakabadhi ghalani wakati akisubiri mazao
yake kuuzwa kwa bei nzuri
Kwa utaratibu mfumo wa stakabadhi ghalani
unasimamamiwa na Bodi ya Maghala ambayo ipo chini ya Wizara ya Viwanda na
Biashara hivyo kuikabili changamoto hiyo serikali imeihamishia Bodi hiyo wizara
ya kilimo ili kupunguza muingiliano uliopo wa kimajukumu katika Wizara hizo
mbili.
Mhe Hasunga amesema kuwa katika mikoa ambayo
tayari vyama vya Ushirika vimeanzishwa mfumo huo unafanya vizuri lakini kwa
mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara, Katavi ambapo vyama vya Ushirika
havijaanzishwa mfumo huo hauwezi kufanya kazi.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga (Mb) ametoa
maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wilaya katika maeneo ambayo hakuna vyama vya
Ushirika vilivyoanzishwa na wananchi wenyewe, Hakuna maghala yaliyosajiliwa, na
Hakuna wenye leseni wanaotambulika na Bodi ya Maghala kutowasumbua wananchi
badala yake wauze kwa uhuru katika maeneo watakayo.
Kadhika, Waziri Hasunga amewataka
wafanyabiashara watakaonunua mazao hayo kwa mzigo unaozidi Tani moja ni lazima
Kodi za Halmashauri zilipwe kwa mujibu wa utaratibu wa kikanuni na kisheria.
Ameongeza kuwa moja ya majukumu ya wakuu wa
Mikoa na Wilaya katika mfumo wa mazao ya Stakabadhi ghalani ni kusimamia
biashara kwa kuzingatia taratibu bila wananchi kudhulumiwa ambapo wasimamizi ni
vyama vya Ushirika, pamoja na Bodi ya Maghani.