
Mshambuliaji wa Manchester United, Odion Ighalo
Na Damian Masyenene
Klabu ya Manchester United ya nchini Uingereza ‘Mashetani
Wekundu’ imefikia makubaliano ya kuendelea kupata huduma ya mshambuliaji raia
wa Nigeria, Odion Ighalo kwa kumuongezea mkataba hadi Januari 31, mwaka 2021.
Ighalo ambaye ni mchezaji wa timu ya Shanghai Shenhua ya
China, yupo kwa mkopo katika klabu ya Manchester United tangu dirisha dogo
mwanzoni mwa mwaka huu, ambapo mkataba wake huo wa mkopo ulitarajiwa kukoma Mei
31, 2020 (mwisho wa msimu) kabla ya kuvurugwa na janga la Corona.
Kwa mujibuwa taarifa zilizochapishwa na kituo cha Sky Sport
cha Uingereza, Mnaijeria huyo ambaye ameichezea United michezo nane katika
mashindano yote na kufunga mabao manne, anatarajiwa kusaini mkataba mpya na
klabu yake ya Shanghai Shenhua utakaodumu hadi 2024 wenye thamani ya Euro 4000
kwa wiki.
Ighalo alijiunga na United kwa mkataba wa muda mfupi katika
siku ya kufunga dirisha dogo la usajili Januari mwaka huu, ambapo lilikuwa
chaguo la Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Ole Gunnar Solskjaer kupata suluhisho la
safu ya ushambuliaji kufuatia mshambuliaji tegemeo, Marcus Rashford kupata majeraha
ya mgongo mwishoni mwa mwaka jana
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464