Header Ads Widget

DKT. ABBASI ATOA MAAGIZO KUELEKEA MCHEZO WA MWADUI NA YANGA JUNI 13




Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi akitoa maelekezo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela juu ya namna ya kufuata miongozo na kanuni za afya kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) baina ya Mwadui FC na Yanga SC.

Na Damian Masyenene - Shinyanga Press Club Blog


KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi leo Jumanne Juni 9, 2020 amefanya ziara mkoani Shinyanga kukagua viwanja vya michezo vya Mwadui, Fresho na CCM Kambarage kujionea namna ambavyo miongozo, maagizo na kanuni za afya juu ya kujikinga na virusi vya Corona inavyotekelezwa.

Katika ziara hiyo, Dkt. Abbasi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali aliwataka wasimamizi wa viwanja kuhakikisha wanazingatia miongozo hiyo ikiwemo kuweka mifumo ya maji tiririka kuhakikisha mashabiki wana nawa kabla ya kuingia uwanjani, kupimwa joto la mwili na kukaa umbali wa mita moja majukwaani.

Dkt. Abbasi akisikiliza maelezo kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela.

Dkt. Abbasi amesema kwa viwanja ambavyo havitazingatia maagizo hayo vitafungwa, huku akibainisha kwamba serikali imetoa onyo kali kwa wasimamizi wa viwanja vya Nangwanda Sijaona na Azam Complex kwa kutofuata masharti ya afya kwenye michezo ya kirafiki iliyofanyika hivi karibuni kwenye viwanja hivyo.

"Hili ni tamko nalitoa hapa Shinyanga lakini ni kwa ajili ya wahusika wote, hiyo Jumamosi tutafuatilia michezo yote kuona kama kanuni tulizoelekeza zinafuatwa, kwa uwanja wowote ambao hautozingatia maagizo haya basi tutasimamisha mchezo na kuufunga uwanja.

"Ni muhimu sasa wasimamizi wa viwanja kuyazingatia hayo waweke mifumo ya maji tiririka ili mashabiki wanawe kabla ya kuingia, wapimwe joto na wakae mita moja majukwaani," alisema.


Akipokea maelekezo hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela amesema tayari wameshakaa na maofisa wa afya, wamiliki wa uwanja na wasimamizi ili kuhakikisha vitendea kazi vinakuwepo na maagizo yote yanafuatwa hususan kwa mchezo wa Jumamosi utakaozikutanisha timu za Mwadui FC na Yanga SC kwenye uwanja wa CCM Kambarage.

"Tunafanya juhudi zote kuhakikisha kabla ya mchezo huo mahitaji yote yanakuwepo, tayari tumeshakutana na pande zote zinazohusika na wameshapewa maelekezo kilichobaki ni kuyatekeleza na naamini mpaka kufikia Jumamosi kila kitu kitakuwa sawa," alisema Msovela.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela akieleza hatua zilizochukuliwa na mkoa huo kuzingatia maagizo ya wataalam wa afya kuelekea mchezo wa jumamosi.

Naye Mjumbe wa Mkutano Mkuu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Msimamizi wa Kanda namba tano inayosimamia mikoa ya Shinyanga na Simiyu, Osuri Kosuri ameeleza kuwa wanaendelea vyema na matayarisho ya uwanja wa CCM Kambarage kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi lakini wakati huo wakiendelea kushirikiana na viongozi wa serikali katika kufanikisha utekelezaji wa kanuni na miongozo ya afya juu ya kujikinga dhidi ya Virusi vya Corona.

Dkt. Hassan Abbasi akisikiliza maelezo kutoka kwa wataalam wa afya juu ya maandalizi yaliyofanywa kwenye uwanja wa CCM Kambarage kuelekea mchezo wa Jumamosi.

Juni 13, mwaka huu, Ligi Kuu Tanzania Bara itarejea rasmi baada ya kusimama kwa takribani miezi miwili kufuatia maambukizi ya Virusi vya Corona, ambapo ligi hiyo itarejea kwa mchezo wa kwanza wa kiporo wa raundi ya 17 ukizikutanisha wenyeji Mwadui FC dhidi ya Wana Jangwani, Yanga SC kwenye dimba la CCM Kambarage, mjini Shinyanga, huku Mwadui FC wakiwa na kumbukumbu nzuri kwenye dimba hilo ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba SC katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.

Mafundi wakiendelea kuufanyia maboresho uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga ikiwa ni maandalizi ya mchezo wa ligi kuu utakaozikutanisha timu za Mwadui FC dhidi ya Yanga SC.
Muonekano wa Uwanja wa CCM Kambarage ukiendelea kufanyiwa maboresho na maandalizi kuelekea mtanange wa Jumamosi.
Picha zote na Damian Masyenene - Shinyanga Press Club Blog