Header Ads Widget

WOMEN FORCE SHINYANGA YATOA MSAADA WA VIFAA KINGA VYA CORONA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA HUO


Mwenyekiti wa Kikundi cha Women Force, Magreth Mambali akimkabidhi Boksi la Barakoa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya COVID - 19 katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga#.

KIKUNDI cha Wanawake ‘ Women Force’ kinachojihusisha na Masuala ya Hisa na Kusaidia Jamii kimetoa msaada wa vifaa kinga vyenye Thamani ya Shilingi 700,000/= katika mapambano ya Maambukizi ya Virusi vya Corona (COVID -19) katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga.

Vifaa hivyo vimekabidhiwa Mei 22,2020 na Mwenyekiti wa Kikundi cha Women Force, Magreth Mambali kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga.

Vifaa vilivyotolewa na Kikundi cha Women Force kilichopo katika Manispaa ya Shinyanga chenye wanachama 15 ni pamoja na Stendi mbili za Kisasa ya kunawia mikono bila kugusa koki,Barakoa 150, Gloves 200 na sabuni 36 za kunawia mikono vyote vikiwa na Thamani ya Shilingi 700,000/=.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Women Force, Magreth Mambali amesema wanachama wa Kikundi hicho na wadau wengine wameamua kuchangishana fedha ili kununua vifaa kinga kwa ajili ya kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika Mapambano dhidi ya COVID – 19.

“Hiki ni kikundi cha Hisa hali kadhalika tunasaidia watu wenye uhitaji katika jamii wakiwemo wazee,yatima na wasiojiweza. Kutokana na huu Ugonjwa wa Corona tumeona ni vyema pia tuchangie kidogo tulichonacho katika Hospitali hii ya Mkoa wa Shinyanga ili kuiongezea nguvu serikali katika kukabiliana na Maambukizi ya Virusi vya Corona”,ameeleza Mambali.

"Msaada huu tumeutoa kwa jamii katika kipindi hiki cha ugonjwa huu wa Korona lakini pia kama njia moja wapo ya kutoa sadaka katika kipindi hiki cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani" ,ameongeza mhasibu wa kikundi cha Women Force Bi. Mwajuma Osmani.

Naye Katibu wa Kikundi cha Women Force, Liku Ndaki amesema Kikundi hicho kinaundwa na wanawake wafanyabiashara na wafanyakazi serikali na taasisi binafsi.

Akipokea vifaa hivyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile amekishukuru Kikundi cha Women Force mchango huo wa vifaa waliotoa katika mapambano dhidi vya Ugonjwa wa Corona.

“Hivi vitu mlivyotupa ni vya muhimu sana kwetu,ni msaada mkubwa sana mmetusaidia ili kuhakikisha mapambano dhidi ya Corona yanaenda sambamba na maelekezo ya serikali kwani ukiachia mbali watu wanaokuja kuhudumiwa na kuona wagonjwa lakini kuna wastani wa watumishi 300 katika Hospitali yetu Rufaa ya mkoa, hivyo tutaweka vituo vingine zaidi vya kunawia mikono ambavyo watu watakuwa wananawa mara kwa mara wawapo hospitalini”, amesema Dkt. Ndungile.


Mwenyekiti wa Kikundi cha Women Force, Magreth Mambali akionesha ya kunawa mikono kwa kutumia Stendi ya kisasa ya kunawia mikono akikabidhi vifaa vya kujikinga na COVID - 19 kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya COVID - 19 katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga.


Mwananchi aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga akinawa mikono getini kwa kutumia Stendi ya kisasa ya kunawia mikono bila kugusa ambayo ni sehemu ya stendi mbili zilizotolewa na Kikundi cha Women Force ili kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Corona katika hospitali hiyo.


Kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile akikishukuru Kikundi cha Women Force kwa kuchangia katika mapambano dhidi ya COVID - 19.

Wanachama wa Kikundi cha Women Force wakipiga picha ya kumbukumbu.