Header Ads Widget

KATIBU MKUU WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA AKAGUA MAENEO YA UWEKEZAJI KAHAMA MJI

Kaibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Profesa Riziki Shemdoe Akikagua na kuongea na                     wajasiriamali eneo la Zongomela Dodoma Halmashauri ya Mji wa Kahama.


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mh. Zainab Telack Akimuonesha katibu Mkuu  Wizara ya Viwanda na                                                   Biashara  Profesa Riziki Shemdoe  eneo la uwekezaji Kahama 

Na DAMIAN MASYENENE - KAHAMA

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe amefanya ziara ya siku moja wilayani Kahama Mkoani Shinyanga na kukagua maeneo mbalimbali ya uwekezaji yaliyotengwa na halmashauri hiyo kwa ajili ya viwanda, wajasiriamali wadogo na uwekezaji utakaofanywa na wizara hiyo.


Katika ziara hiyo ambayo ameambatana na wataalam kutoka Wizara hiyo pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, Katibu Mkuu huyo amekabidhiwa eneo la ekari 62 na Halmashauri ya Mji wa Kahama iliyotolewa bila malipo kwa ajili ya uwekezaji na ujenzi wa kituo maalum (Center of excellence) cha utafiti na Maendeleo ya mazao hususan Pamba katika eneo la Uwekezaji EPZA lililopo Nyashimbi Kata ya Mhongolo mjini humo.

Aidha Profesa Shemdoe ametembelea pia eneo la wajasiriamali na viwanda vidogo la Zongomela lenye ukubwa wa ekari 500 linalojumuisha wajasiriamali zaidi ya 1,500, huku pia akikagua ujenzi wa kiwanda cha vinywaji baridi na vifungashio cha KOM Food Products Co. ltd kinachojengwa eneo la Chapulwa ambacho kikikamilika kitatoa ajira za kudumu 200 na za muda 2,000.

Katibu Mkuu ameipongeza  halmashauri hiyo na kuzitaka halmashauri zingine nchini kuiga mfano huo wa kutenga maeneo ya uwekezaji yatakayotolewa bure kwa ajili ya maendeleo na utekelezaji wa Sera ya viwanda na uchumi, huku akizitaka taasisi za huduma kufikisha huduma kwenye maeneo ya uwekezaji kwa wakati ili kuyawezesha kuanza uzalishaji na kuchangia mapato kwa Taifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mh. Zainab Telack amesesema kuwa eneo la Zongomela lina mchango mkubwa kwa maendeleo ya viwanda mkoani humo, ambapo tayari wameanza mipango ya kutatua baadhi ya changamoto zinazolikabili eneo hilo ikiwemo barabara yenye urefu wa Kilomita 14.5 ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami mwaka huu na pia watatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za SIDO na Maliasili katika eneo hilo ili kusogeza huduma za ushauri wa kitaalam kwa wajasiriamali hao.