Mkurugenzi mtendaji
wa Kampuni ya Nyanhembe Agricultural Farm Khamis Mgeja akiwa katika harakati za kupiga mpunga
Khamis Mgeja
akimsaidia Salma Kazinza mkazi wa Nyanhembe kusukuma baiskeli iliyobeba mpunga
kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara.
Na Paul Kayanda,Kahama
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Nyanhembe Agricultural Farm Khamis
Mgeja inayojishughulisha na shughuli za Kilimo na Ufugaji, ameipongeza serikali
kupitia wizara ya kilimo kutokana na kuliagiza shirika la kuhifadhi chakula
NFRA kununua mazao mbalimbali ya wakulima badala ya kununua mahindi pekee.
Mgeja ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa
wa Shinyanga(CCM) amesema uamuzi huo utatenda haki kwa wakulima wote
wanaojituma katika kulima mazao mbalimbali ya chakula na biashara tofauti na
kipindi kilichopita.
Ametoa pongezi hizo baada ya kutembelewa na waandishi wa habari
kutoka vyombo mbalimbali vya Habari katika shamba lake la mpunga, lililopo
Kijiji cha Nyanhembe Kata ya Kilago wilayani Kahama.
Mgeja amesema wakulima wamemsikia na kumuona hivi karibuni
Waziri wa kilimo Japhet Hasunga akiwa Mkoani Manyara akitoa maelekezo kwa NFRA kununua
mazao yote yanayolimwa na wakulima likiwamo zao la mpunga.
Mkurugenzi huyo wa kampuni ya Nyanhembe Agricultural Farm
alisema uamuzi huo wa serikali utakuwa mwarobaini wa kuwasaidia wakulima kupata
bei nzuri katika mazao yao pamoja na wafanyabiashara wanaonunua mazao kutoa bei
nzuri.
Amesema katika msimu huu amelima ekari 73 ambapo anatarajia
kupata mavuno ya gunia za mpunga 1430, ambapo mpaka sasa tayari amevuna gunia 320
huku akitaja lengo lake kuu katika msimu ujao ni kulima ekari 250.
Hata hivyo Mgeja amedai kuwa kwa sasa ameamua kupumzika siasa na
kubainisha kwamba kwa sasa amejielekeza katika kilimo na ufugaji wa ng’ombe,mbuzi
na ufugaji wa nyuki pamoja na samaki.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464