Header Ads Widget

WMA YAZITAKA HALMASHAURI KUTENGA VITUO VYA MAUZO VIJIJINI KUWAOKOA WAKULIMA NA WIZI


 Picha. Wakulima wakivuna mpunga shambani

Na Damian Masyenene

Shinyanga

Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Shinyanga imesema kuwa ili kuwasaidia wakulima wa mazao mbalimbali nchini kutodhulumiwa na kuibiwa kwenye vipimo na madalali (wanunuzi) wakati wa mauzo, ni vyema halmashauri zikatenga vituo maalum (buying centres) katika maeneo ya vijijini ambapo wakulima watakuwa na vipimo vyao wenyewe.


Ushauri huo umetolewa juzi mjini Shinyanga na Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) mkoa wa Shinyanga, Hilolimus Mahundi katika ofisi zake alipokuwa akizungumzia kaguzi mbalimbali zilizofanyika hivi karibuni na mikakati ya kuwasaidia wakulima wasiendelee kuibiwa wakati huu wa mauzo ya mazao ya mahindi na mpunga yaliyovunwa kwa wingi mkoani hapa.

Mahundi alisema kuwa endapo kama kila kijiji kitakuwa na kituo cha mauzo na mzani wake basi watakomesha wizi na udanganyifu wa vipimo unaofanywa na madalali, ambapo alieleza kuwa kwa sasa kwenye zao la Dengu na Pamba kuna nafuu kwa sababu yanauzwa kupitia ushirika lakini kwa wakulima wa Mpunga na Mahindi bado wamesahaulika.

“Wakulima wa mazao wanaibiwa sana kwahiyo ili wasaidiwe inabidi halmashauri zitenge vituo vya manunuzi ambako wakulima watakuwa na mizani yao iliyohakikiwa kuliko kutegemea ya madalali wanaosaka faida,” amesema.

Katika hatua nyingine Mahundi alibainisha matokeo ya ukaguzi maalum wa vipimo na ufungashaji wa sukari uliofanyika wilayani Kahama kuanzia Mei 5 hadi 13, mwaka huu na kufanikiwa kukamata na kuzuia mizani 27 iliyokuwa inauzwa bila kuhakikiwa na wakala huo, ambayo ingetumika kuwaibia wananchi.

"Tulikamata wafanyabiashara sita kwa makosa ya kuuza mizani ambayo haijahakikiwa na wakala wa vipimo wakiwauzia wafanyabiashara wadogo kienyeji, ambapo walitozwa jumla ya faini ya Sh Milioni 2.3.

“Tunaomba wafanyabiashara wawe waaminifu na wafuate sheria za vipimo ili sisi tusiwe vikwazo kwao, ili kuendelea kuwalinda wananchi na wateja tutaendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara ili mkulima apate fedha inayolingana na thamani ya mazao yake,” alisema.