Header Ads Widget

WATUMISHI WANNE KISHAPU KUFUKUZWA KAZI KWA TUHUMA ZA UPOTEVU WA MILIONI 20.



Na Suzy Luhende

Shinyanga

Kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga kimeazimia kuwafukuza Kazi watumishi  wanne wa halmashauri hiyo baada ya kubainika kuhusika na upotevu wa fedha  Sh milioni 20 na makosa ya nidhamu na utoro kazini .

Akizungumzia maamuzi hayo yaliyoazimiwa Mei 19 mwaka huu, Mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu, Boniface Butondo amesema watumishi hao wamekosa nidhamu ya utumishi wa umma wakiwa kazini baada ya kuonekana kuhusika na upotevu wa fedha za Serikali licha ya kutakiwa kuzirejesha.

Amewataja watumishi hao kuwa ni Ally Mussa  aliyekuwa Mtendaji wa Kijiji cha Pumbula Kata ya Songwa,Njile Kwilasa aliyekuwa Mtendaji wa Kijiji cha Mihama Kata ya Lagana,Marimu Manyirizu kutoka idara ya mifugo ambaye amekuwa mtoro kazini kwa muda mrefu zaidi ya siku 100 na  hajulikani alipo.

Mwingine ni Nkonya Charles  aliyekuwa Mtendaji wa Kijiji cha Talaga wilayani humo,ambapo Butondo amewataka  watumishi wote wafanye kazi kwa bidii na uaminifu.

“Halmashauri tutaendelea na utaratibu wa kuwafukuza na kuwasimamisha kazi watumishi wote wanaokwenda kinyume na maadili ya kazi zao,ili kuhakikisha kuna kuwa na nidhamu na kuzuia upotevu wa fedha za serikali''alisema Butondo.

Aidha Mwenyekiti huyo amefafanua kuwa kabla ya maamuzi hayo watumishi hao waliitwa na kutakiwa kurejesha fedha kwa wakati na tayari wamefikishwa kwenye kamati lakini hawajarudisha na kulilazimu baraza kufikia maamuzi hayo.

Baadhi ya madiwani akiwemo Frednand Mpogomi na Felister Nkinga wamepongeza maamuzi hayo kwani watumishi hao walipewa nafasi ya kurudisha fedha hizo lakini hawakutekeleza hadi leo.

Tazama picha mbalimbali za  kikao hicho