Header Ads Widget

ROBO FAINALI FA: SIMBA DHIDI YA AZAM FC, YANGA YATUPWA KWA KAGERA SUGAR





Na Damian Masyenene

Droo ya mechi za robo fainali kombe la shirikisho la Azam (Azam Sport Federation Cup) maarfu kama FA imepangwa leo Mei 29, 2020 katika ofisi za Azam jijini Dar es Salaam na mabingwa watetezi wa kombe hilo, Azam FC kupangwa na wekundu wa Msimbazi, Simba SC.

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa kati ya Juni 27 na 28 mwaka huu kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam, Simba wakiwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) na Wana lambalamba Azam FC wakitetea ubingwa wa kombe la FA.

Michezo mingine itakayopigwa katika hatua hiyo ya robo fainali ni Mabingwa wa Kihistoria Wana Jangwani, Yanga SC watakaomenyana na Wanankurukumbi Kagera Sugar, huku Namungo FC wakiikaribisha Alliance FC ya Mwanza.

Nayo timu pekee iliyofuzu hatua hiyo kutoka daraja la kwanza, Sahare All Stars ya Tanga itakuwa mwenyeji wa Wanakuchele Ndanda FC, ambapo michezo yote ya hatua hiyo ya robo fainali itachezwa jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Taifa, Uhuru na Azam Complex Chamazi.

Michezo ya hatua ya nusu fainali inatarajiwa kuchezwa mwezi Julai, mwaka huu ambapo mshindi kati ya Namungo FC na Alliance FC atakutana na mshindi wa mchezo baina ya Sahare All Stars na Ndanda FC, huku mshindi kati ya Simba SC na Azam FC akikutana na mshindi kati ya Yanga SC na Kagera Sugar.

Fainali ya mchuano hiyo itapigwa Julai, 2020, ambapo bingwa wa kombe la FA ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa ya kombe la shirikisho ngazi ya vilabu barani Afrika (CCC).