
Michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) imetangazwa
kuanza tena rasmi Juni 13, mwaka huu baada ya kusimama kwa takribani miezi
miwili kutokana na janga la virusi vya Corona.
Uamuzi huo ulitangazwa jana Mei 28 mwaka huu jijini
Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almas Kasongo katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari ikiwa ni mwitikio wa agizo la serikali
kurejesha shughuli za michezo nchini ifikapo Juni mosi mwaka huu.
Kasongo katika taarifa yake amesema kuwa mechi za ligi
kuu ya Vodacom msimu wa 2019/2020 zitaendelea kuchezwa kuanzia Juni 13, 2020,
ambapo ratiba itatangazwa Jumapili Mei 31, mwaka huu.
Ikumbukwe Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na
Michezo kupitia kwa waziri Dk. Harrison Mwakyembe iliweka wazi kuwa michezo
yote ya Ligi Kuu itachezwa jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Uhuru, Taifa
na Azam Complex.
Wakati huo huo, Serikali imetoa mwongozo wa
kuzingatiwa wakati wa kuendesha shughuli za michezo katika kipindi chote cha
mlipuko wa COVID 19 nchini kwa lengo la kudhibiti maambukizi.
Ambapo viongozi wa viwanja wa vyama /shirikisho husika wametakiwa kuweka miundombinu ya kuwezesha upatikanaji wa maji tiririka na sabuni kwa ajili ya kunawia mikono au vitakasa mikono(sanitizer)katika maeneo yote muhimu kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.
Na Damian Masyenene
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464