
Na Damian
Masyenene - Shinyanga Press Club blog
Jeshi la Polisi nchini kupitia kitengo maalum cha
operesheni cha jeshi hilo limetangaza matokeo ya operesheni maalum ya kudhibiti
vitendo vya kiuhalifu ikiwemo wizi wa Pikipiki kwa mikoa Nane ya Kanda ya Ziwa,
ambapo jumla ya mali/pikipiki 825 zidhaniwazo
kuwa za wizi zilikamatwa na kesi 354 kufunguliwa
dhidi ya watuhumiwa waliokamatwa.
Matokeo ya
opreresheni hiyo ya takribani mwezi mmoja iliyoanza Mei 4 hadi 29, mwaka huu ikihusisha mikoa nane ya Mwanza, Geita, Shinyanga,
Simiyu, Tabora, Tarime/Rorya, Mara
na Kagera, imetangazwa leo Mei 30, 2020
jijini Mwanza katika taarifa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Operesheni maalum
za jeshi la polisi, SACP Mihayo Msikhela.
SACP Msikhela amesema
kuwa hali ya usalama katika mikoa hiyo imeendelea kuwa shwari kutokana na
juhudi kubwa inayofanywa na Jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya
ulinzi na usalama pamoja na raia wema.
Taarifa hiyo pia imefafanua namna mashauri ya operesheni
yalivyoshughulikiwa kwa kila mkoa, ambapo Tabora (43), Mwanza (19), Simiyu
(36), Shinyanga (19), Tarime/Rorya 38), Mara (09), Geita (97) na Kagera (92) na
kufanya jumla ya kesi zilizofunguliwa kufikia 353, kesi zilizopelekwa
mahakamani (60), kesi zilizopata mafanikio (12), kesi zilizofungwa polisi (16),
kesi zilizo chini ya upelelezi (287), pikipiki zilizotozwa faini (241), huku
magari sita yakikamatwa.
“Mwanza walikamatwa watuhumiwa 12 na injini za boti 106
katika visiwa vya Juma, Gembale na Zilagula wilayani Sengerema, Tabora
wamekamatwa watatu wa mauaji, Geita
wamekamatwa watuhumiwa wawili wa wizi wa matairi manne ya Gari aina ya Toyota
Surf T 477 ACY. Katika kufanikisha tukio hilo watuhumiwa walitumia
bajaji namba MC 688 BXA TVS KING
kwenye ubebaji wa tairi hizo nayo pia imekamatwa na inashikiliwa ili taratibu
za kisheria ziweze kufuatwa,” amesema Kamanda Msikhela.
Vile vile, amebainisha baadhi ya mambo kadhaa
yaliyobainika katika operesheni hiyo kuwa ni wamiliki wengi wa
vyombo vya moto hususani pikipiki hawana uelewa wakutosha kuhusu umiliki,
utunzaji, kuazima na hata kukodisha kwa mfano mmiliki anamkabidhi mtu pikipiki
bila mikataba au kumjua kiundani anayemkodisha au abiria wake.
“Watu
wanachonga namba za pikipiki ilhali hawana vibali au leseni za kufanya kazi
hizo, mfano kwa mkoa wa Mara wamekamatwa watuhumiwa watatu wanaohusika na
kuchonga namba za pikipiki.
”Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi wote kutoa taarifa za uhalifu
na wahalifu mapema kabla madhara hayajatokea kwani wahalifu wapo kwenye jamii
zetu, hivyo jamii inapaswa kuuchukia uhalifu ili nchi yetu iwe na amani,” amesema.