Na Mwandishi wetu
Askofu wa Kanisa la International
Evangelical Assembly of God Tanzania (IEAGT) la mjini Shinyanga, David Mabushi
amesema kuwa tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli
kuruhusu shughuli mbalimbali nchini kurejea katika hali ya kawaida ifikapo Juni
mosi, mwaka huu siyo ya kukurupuka na hailipeleki taifa katika moto wa ugonjwa
wa Corona.
Mei 21, mwaka huu Rais Magufuli
alilitangazia taifa kuwa shughuli mbalimbali yakiwemo masomo ya vyuo na kidato
cha sita pamoja na michezo ya ligi kuu, daraja la kwanza na la pili vitarejea
ifikapo Juni Mosi, mwaka huu baada ya kusimama kwa takribani miezi miwili
kupisha maambukizi ya Virusi vya Corona.
Ambapo kufuatia tamko hilo,
Askofu Mabushi akizungumza na waumini wake leo katika ibada ya ijumaa amewataka
kusherekea tamko hilo kwa kuwa ni ishara ya kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa wa
Corona kutokana na maombi ambayo Mungu
amejibu kwa taifa letu.
Mabushi amesema kuwa Rais Dk.
Magufuli hajakurupuka kwa tamko alilolitoa jana kwani amefanya utafiti wa
kutosha na amejua ukweli halisi wa hali ilivyo kwa kupata taarifa mbalimbali
kutoka kwa watendaji wake.
“Naamini kuwa Rais na Serikali
yake hawezi kukubali kuliingiza taifa katika moto mkubwa wa Corona kama hana
mapenzi na wananchi wake,” alisema Askofu Mabushi.
Kwa upande mwingine Askofu
Mabushi aliwaomba waumini wa kanisa hilo kufanya maombi ya kumshurukuru
Mwenyezi Mungu kwa kuwa amejibu maombi ambayo waliomba tangu mwanzo wa janga
hilo kuripotiwa na kupelekea Serikali kufunga baadhi ya shughuli zenye
mikusanyiko ya watu na kuacha uhuru wa nyumba za ibada kuendelea kumcha Mungu
ili kuvusha taifa katika vita ya ugonjwa huo.
Pia amewaasa wanafunzi kwenda
kuongeza jitihada zaidi ya masomo yao pindi watakaporudi mashuleni ili
kukamilisha malengo yao ya kimasomo na wasome bila hofu na kujikita zaidi
katika kufata kanuni za afya na usafi ili wakamilishe masomo yao kwa amani.