#MKURUGENZI MKUU AWATAKA MAMENEJA KUSIMAMIA MIRADI IPASAVYO
Arusha
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mha. Wolta Kirita amefanya ukaguzi wa miradi ya maji ya Minjingu - Oltukai na mradi wa vijiji vinne Makuyuni (Makuyuni, Naiti, Mbuyuni na Losimingori) inayotekelezwa katika wilaya ya Monduli mkoani Arusha, ikiwa ufuatiliaji wa Utekelezaji wa miradi na utekelezaji wa maagizo ya viongozi.
Akiongea na wananchi wa kijiji cha Oltukai mara baada ya kukagua mradi wa Minjingu - Oltukai ambao umeanza kutoa maji, Mha. Kirita amewataka wananchi hao kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu hiyo.
"Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatumia fedha nyingi sana kuhakikisha kila kijiji kinapata maji safi na salama. Maji yakifika kwenu, jukumu letu sisi RUWASA limeisha kwa asilimia 80, asilimia 20 iliyobaki ni yenu wananchi kuhakikisha mnalinda miundombinu hii isiharibiwe kiholela ili idumu kwa vizazi na vizazi," alisema Mha. Kirita.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Oltukai Bwana Rudda Kilusu ameishukuru RUWASA kwa kuwapelekea maji katika eneo hilo ambalo kwa muda mrefu lilikuwa na changamoto kubwa ya maji na kumuhakikishia Mkurugenzi Mkuu kuwa viongozi wa kijiji hicho na wananchi watailinda miundombinu hiyo kwa nguvu zote.
Wananchi wa Kijiji cha Oltukai nao hawakuficha furaha yao baada ya kupata huduma hiyo muhimu.
" Kwa kweli tumefurahi kupata maji katika kijiji chetu kwani kwa sasa hatuhangaiki tena kutafuta maji umbali mrefu na pia kabla ya RUWASA kuleta maji tulikuwa tunachota maji makorongoni, maji ambayo sio salama hali iliyopelekea watoto wetu kuumwa matumbo na hata shuleni wanafunzi walikuwa wanatembea umbali mrefu kutafuta maji ya kupikia lakini hali hiyo kwa sasa hakuna", Alisema Bi. Agness Laizer, mkazi wa Oltukai.
Akiwa katika mradi wa Vijiji Vinne vya Makuyuni (Makuyuni, Naiti, Mbuyuni na Losimingor), Mhandisi Kirita alijionea jinsi mkandarasi wa mradi huo kampuni ya SKY WARDS inavyofanya kazi kwa kasi na kumuhakikishia Mkurugenzi Mkuu kuwa ndani ya siku ishirini kuanzia tarehe 30 Septemba, maji yataanza kuwafikia wananchi wa kijiji cha kwanza kati ya vijiji vinne vya Mradi.
Akihitimisha ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mha. Kirita aliwataka Mameneja wa Mikoa nchi nzima kushirikiana kwa karibu na Mameneja wa Wilaya na kufanya kazi kama timu moja ili kuhakikisha kila shilingi inayotolewa kwa wakandarasi inatumika ipasavyo na wananchi wanapata maji kama ilivyokusudiwa.
"Sisi RUWASA hatuna sababu ya kumuacha Mkandarasi afanye kazi peke yake, kila Meneja wa mkoa na wilaya ahakikishe kazi inafanyika vizuri. Maelekezo ya Mheshimiwa Waziri ni kuwa maji si anasa, maji ni haki na ndani ya siku 20 wananchi wa Makuyuni lazima waanze kunywa maji na hakuna mchezo kwenye hili," alisisitiza Mha. Kirita.
Ziara hiyo ya Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA mkoani Arusha ni muendelezo wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi na utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya Viongozi.





