` DIWANI WA NGOKOLO JACKLINE ISARO AONGOZA WANANCHI KUCHIMBA MSINGI UJENZI WA ZAHANATI

WANDAMAN HOTEL

DIWANI WA NGOKOLO JACKLINE ISARO AONGOZA WANANCHI KUCHIMBA MSINGI UJENZI WA ZAHANATI

 


Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA

Diwani wa Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga Jackline Isaro, amewaongoza wananchi wa kata hiyo katika zoezi la uchimbaji wa msingi wa ujenzi wa zahanati itakayohudumia zaidi ya wakazi 2,000.

TAZAMA VIDEO👇👇


Zoezi hilo limefanyika leo Septemba 19, 2026, huku likitarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2027. Hatua hiyo inalenga kumaliza changamoto ya wananchi kufuata huduma za matibabu katika maeneo ya jirani kutokana na uhitaji wa huduma hiyo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Diwani huyo amesema ujenzi huo unatarajiwa kugharimu Sh. milioni 128, ukihusisha vitendeakazi, mafundi pamoja na mahitaji mbalimbali yatakayokamilisha shughuli za ujenzi huo.

Sambamba na hilo ,Jackiline amesema uongozi wa Serikali ya Kata hiyo, kwa kushirikiana na viongozi wa mtaa, unaendelea kutatua changamoto za wananchi katika kata hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi na ahadi kupitia kampeni za uchaguzi alizozitoa kwa wananchi hao.
“Kinachoendelea kwa sasa ni kwa mujibu wa ilani ya Chama cha Mapinduzi na ahadi zangu nilizozitoa kwa wananchi wa kata hii. Niwaahidi tu kuwa serikali hii itaendelea kutatua changamoto awamu kwa awamu,” amesema Jackline.

Mbali na hilo, Diwani huyo amesema uongozi wa kata hiyo unaendelea na jitihada za kukabiliana na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha mwanzoni mwa mwezi Oktoba, huku akiwasihi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kukabiliana na janga hilo.
“Sisi kama viongozi, jukumu letu ni kusimamia hatua za kukabiliana na mvua hizi, japo tunawakumbusha wananchi wetu kuendelea kuweka mazingira rafiki katika makazi yao,” amesema Jackline.

Nao baadhi ya wananchi kutoka kata hiyo waliojitokeza katika zoezi la uchimbaji wa msingi wa zahanati hiyo, akiwemo Jackson Masingija na Zera Sengimluka, wamepongeza hatua iliyofikiwa na serikali ya kusogeza huduma za afya katika kata hiyo, hali itakayowaondolea adha ya kufuata huduma za matibabu nje ya kata hiyo.
“Tunaishukuru serikali yetu kwa kutazama changamoto tunazokutana nazo katika kupata huduma za afya. Awali tulikuwa tunapata tabu, hasa mgonjwa anapohitaji huduma ya haraka,” walisema wananchi hao.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Kata ya Ngokolo ina jumla ya wakazi 25,000, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka zaidi.

TAZAMA PICHA👇👇
Diwani wa Ngokolo Manispaa ya Shinyanga Jackline Isaro akiongoza wananchi kuchimba Mtaro ujenzi wa Zahanati.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464