` MRADI WA MAJI WA BARRICK NORTH MARA KUNUFAISHA ZAIDI YA WAKAZI 125,000 TARIME

WANDAMAN HOTEL

MRADI WA MAJI WA BARRICK NORTH MARA KUNUFAISHA ZAIDI YA WAKAZI 125,000 TARIME

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (katikati), akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa mradi wa pili wa chanzo cha usambazaji wa maji safi na salama Nyamongo wilayani Tarime , kushoto ni Meneja wa Barrick North Mara , Apolinary Lyambiko na kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime , Juster Magabe. 
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (katikati), akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa mradi wa pili wa chanzo cha usambazaji wa maji safi na salama Nyamongo wilayani Tarime. Kushoto ni Meneja wa Barrick North Mara , Apolinary Lyambiko na kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime , Juster Magabe.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele akisoma maandishi wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi wa pili wa chanzo cha usambazaji wa maji safi na salama Nyamongo wilayani Tarime.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele akifungua maji mara baada ya uzinduzi huo wa mradi awamu ya pili , Nyamongo , wilayani Tarime mkoani Mara. 

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele akimtwisha mama ndoo kichwani mara baada ya kuzindua mradi wa chanzo cha usambazaji maji safi na salama , Nyamongo , Tarime mkoani Mara. 

Mkuu wa Wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele akizungumza kwenye mradi wa chanzo cha usambazaji maji safi na salama , Nyamongo , Tarime mkoani Mara. 

Mkuu wa Wilaya ya Tarime , Meja Edward Gowele akiwa na wananchi wa Nyamongo baada ya uzinduzi wa mradi wa usambazaji maji safi na salama. 


MGODI wa Dhahabu wa Barrick North Mara umekabidhi rasmi awamu ya pili ya mradi wa upanuzi wa chanzo cha usambazaji wa majisafi na salama utakaonufaisha zaidi ya wakazi 125,500 wananchi katika kijiji cha Kewanja kilichopo jirani na mgodi huo .

Mradi huu  umetekelezwa kwa fedha za Uwajibikaji kwa jamii (CSR) kiasi cha shilingi bilioni 2.665 kwa ajili ya upanuzi wa chanzo cha maji cha Nyamongo, wilayani Tarime vijijini kilichopo ndani ya eneo la Mgodi ambacho awali kilisanifiwa kuhudumia wananchi 27,742 wa vijiji vya Nyangoto, Matongo, Mjini Kati na Nyabichune.

Kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji katika vijiji vingine saba vinavyozunguka mgodi, chanzo hiki kilisanifiwa upya kwa lengo la kuhudumia wananchi 125,566 katika vijiji vingine sita vya Genkuru, Nyamwaga, nyakunguru, Kerende, Msege na Komarera.

Akiongea wakati wa hafla ya kukabidhi mradi huo mwishoni mwa wiki, Meneja wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, alisema awamu ya pili iliyokamilika na kukabidhiwa inahusisha kilomita 5.5 za bomba kuu la kusafirisha maji na kilomita 8.6 za mtandao wa usambazaji na kuongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo ni hatua muhimu katika kuboresha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi wa vijiji 11 vinavyozunguka mgodi.

 “Kwetu kama mgodi, maji ni zaidi ya huduma, ni rasilimali muhimu inayogusa maisha, afya, uchumi na ustawi wa wananchi. Tunajivunia kuwa sehemu ya juhudi za serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama,” amesema Lyambiko.

Amesema tangu mwaka 2019 Barrick North Mara imekuwa ikitenga wastani wa shilingi bilioni nne kila mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo ya maji, elimu, afya, miundombiunu ya barabara, mazingira na uwezeshaji kiuchumi hasa kwa vijana.

Awali, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tarime, Mhandisi Leo Respicius, amesema maji ya mradi huo yamethibitishwa na vipimo vya kitaalamu kuwa ni safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

 “Kukamilika kwa mradi huu ni ushuhuda mwingine wa jinsi mgodi wa Barrick North Mara unavyotekeleza azma yake ya kuwa mshirika wa maendeleo kwa jamii inayozunguka mgodi na wilaya ya Tarime kwa ujumla,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Gowele, ameushukuru Mgodi wa Barrick North Mara kwa kuendelea kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kijamii kwa vitendo kupitia sera na kanuni ya uwajibikaji kwa jamii (CSR).

 “Tumefurahi kuzindua huu mradi wa maji hapa. Niwapongeze na kuwashukuru Barrick kwa namna ambavyo inashirikiana na serikali kutekeleza miradi ya kijamii kupitia mpango wao wa CSR,” amesema.

 Meja Gowele alisema utekelezaji ya miradi hiyo unaenda sambamba na maelekezo ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. “Mhe. Rais Samia anataka huduma ya maji kwa wananchi ifike kila kona,” amesisitiza.

Aliwataka wakazi wa kijiji cha Kewanja kutunza mradi huo ili uwe endelevu kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.

Aidha, Meja Gowele amewasihi wananchi wanaozunguka mgodi wa North Mara kuendelea kuunga mkono mgodi huo ili waendelee kufurahia na kunufaika zaidi na uwekezaji huo.

Maria Polycarp, ni mama wa watoto watatu, mkazi wa Kijiji cha Nyamongo akiongelea juu ya kukamilika kwa mradi huu alisema kwa miaka mingi tangu akiwa msichana, alizoea kuamka alfajiri kufuata maji mbali na hiyo ilikuwa ndiyo ratiba yake ya kila siku.

 Anasema shida hiyo ilimwathiri yeye na wanakijiji wenzake kwa miaka mingi.

Lakini, anasema hivi sasa yeye ni mwenye kicheko na furaha ya ajabu, kutokana na shida hiyo ya maji kutatuliwa. Anaeleza kuwa Barrick North imewezesha waanze kupata maji safi na salama katika kupitia mradi ambao sasa umefikia vijiji 11  na kufanya kero ya maji kuwa historia.
 
“Tulikuwa tunateseka kwa shida ya maji, lakini sasa tutaokoa muda kwa kufanya shughuli zingine za kiuchumi. Tunaishukuru Barrick North Mara kwa kuleta majisafi kwenye makazi yetu hapa Nyamongo na kwenye vijini vingine vinavyozunguka Mgodi”, amesema Maria huku akitabasamu.

Naye Diwani wa kata ya Kemambo kilipo kijiji cha Kewanja, Rashid Bogomba, amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na kuboresha mahusiano mema na Mgodi wa Barrick North Mara.

 “Kitu kama hiki [mradi huu wa maji] tungekisubiri kwa miaka mingi lakini leo tumekipata kwa urahisi kupitia Mgodi wa Barrick North Mara. Tuendelee kuwapa ushirikiano watu wa Barrick na hii itatusaidia sana,” alisema Bogomba ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) ya Barrick North Mara.

Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime nao wameonesha kufurahishwa na mradi huo wa maji na mingine inayotekelezwa na mgodi huo kupitia mpango wake wa CSR.

 “Tumefurahishwa sana na mradi huu na tunatambua kazi nzuri inayofanywa na kampuni ya Barrick na halamshauri tutaendelea kuwapa ushirikiano mzuri,” amesema Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Juster Magabe.

Nao wananchi na viongozi wengine wa kijamii waliohudhuria hafla hiyo walisema mradi huo utawaondoa adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji katika vyanzo ambavyo sio salama na uhakika.

Kufika kwa maji karibu na makazi ya wananchi kunawapunguzia wanawake adha ya kutembea umbali mrefu, na hivyo kupata muda wa kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na kukuza uchumi wa kaya.







Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464