` AZZA: IMESELA KUPATA MAJI KUPITIA MRADI WA ZIWA VICTORIA

WANDAMAN HOTEL

AZZA: IMESELA KUPATA MAJI KUPITIA MRADI WA ZIWA VICTORIA


Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, akisalimiana na wacheza ngoma wakati wa ziara yake katika Kijiji cha Imesela. Picha na Stela Paul
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, akiwa na Diwani wa Kata ya Imesela, Mheshimiwa Seth Msangwa, wakizungumza kwa pamoja wakati wa ziara yake katika Kijiji cha Imesela. 
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, akiwa na Diwani wa Kata ya Imesela, Mheshimiwa Seth Msangwa, wakifurahia jambo wakati wakicheza ngoma ya Ugoyangi, ngoma ya asili inayohusisha kucheza na nyoka. 
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, akizungumza na wananchi wakati wa mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Imesela.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, akizungumza na wananchi wakati wa mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Imesela.
Diwani wa Kata ya Imesela, Mheshimiwa Seth Msangwa, akizungumza na wananchi wakati wa mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Imesela.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Said Nassoro, akiwa amembeba nyoka wakati wa burudani ya ngoma ya Ugoyangi katika Kijiji cha Imesela.

Na Stela Paul – Imesela, Shinyanga

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, amesema utekelezaji wa mradi wa maji ya Ziwa Victoria unaoendelea katika Kijiji cha Imesela, Kata ya Imesela, Wilaya ya Shinyanga, unalenga kumtua ndoo mama kichwani pamoja na kuchochea shughuli za maendeleo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Azza amesema hayo Oktoba 3, 2026, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo, ambapo ametolea ufafanuzi changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa kijiji hicho, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kijiji kwa kijiji katika Jimbo hilo.

"Vijiji vyote vya Kata ya Imesela, kikiwemo kijiji hiki, vinakwenda kupata maji kupitia tenki lililojengwa ndani ya kijiji hiki. Ninavyofahamu, hatua inayofuata ni kuchukua maji kutoka kwenye chanzo kikuu cha Zobogo ili yaweze kufika kwenye tenki na mabomba yasambazwe katika vijiji vyote vya Imesela," amesema Azza.

Aidha, katika sekta ya afya, Mbunge huyo ameahidi kwamba baada ya kukamilika kwa ujenzi wa boma la zahanati ya kijiji hicho, unaojengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na fedha za Jimbo, atabeba jukumu la kuhakikisha jengo hilo linapauliwa na kukamilika ili liweze kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Mbunge Azza amevitaka vikundi vilivyopo katika Kijiji cha Imesela kuwa na miradi rasmi ya uwekezaji ili viweze kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, akieleza kuwa fedha hizo hutolewa kwa lengo la kukuza miradi iliyopo na siyo kuanzisha miradi.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Imesela ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mheshimiwa Seth Msangwa, amesema ataendelea kuwasilisha kwa Mbunge huyo changamoto mbalimbali za maendeleo zilizopo katika kata hiyo ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi.




































Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464