WANACHAMA WA MISA TANZANIA WATEMBELEA DARAJA LA MAGUFULI LA KIGONGO- BUSISI, AMBALO LIMETAJWA KUCHOCHEA MAPINDUZI YA KIUCHUMI
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Daraja la Magufuli la Kigongo–Busisi limetajwa kuwa kichocheo kikubwa cha shughuli za kiuchumi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani, kutokana na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, ambapo awali, watumiaji wa vivuko walitumia hadi saa mbili kuvuka, lakini kwa sasa safari hiyo huchukua dakika tano tu kupitia daraja hilo.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 13, 2026, na Msimamizi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Jijini Mwanza Mhandisi William Sanga, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao ni wanachama wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN) waliotembelea daraja hilo.
Amesema, moja ya manufaa makubwa ya daraja hilo ni kuchochea shughuli za kiuchumi, kwa kuwa ni kiungo muhimu kinachorahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, hasa katika shughuli za kibiashara.
Aidha, amesema daraja hilo linaunganisha wilaya mbili za Misungwi na Segerema, na kwamba lipo katika ushoroba wa Ziwa Victoria, ambao unaoanzia Sirari mpakani mwa Tanzania na Kenya, na kuunganisha maeneo mengine ya nchi jirani, ikiwemo Uganda.
“Daraja hili ni refu zaidi Afrika Mashariki na Kati, likiwa na urefu wa kilomita tatu, ambapo upande mmoja una kilomita 1.5 na upande mwingine kilomita 1.5,” amesema Mhandisi Sanga.
Aidha, amesema daraja hilo lilianza kujengwa Februari 25,2020 na Mwaka jana 2025 lilikamilika na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alilizindua.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha utekelezaji wa mradi huo, zilitengeneza ajira takribani 29,000, huku akitaja gharama za ujenzi hadi kukamilika kwake zikifikia zaidi ya Sh. bilioni 700.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa MISA TAN Edwin Soko, amesema ziara hiyo imelenga kutembelea miradi ya kimkakati, ili kuwawezesha waandishi wa habari kuandika na kutoa taarifa sahihi kuhusu miradi hiyo kwa umma.
Aidha, ameshauri Serikali kuendelea kuwashirikisha waandishi wa habari katika ziara za kutembelea miradi ya kimkakati, ili wawe mabalozi wazuri wa kuitangaza na kueleza manufaa yake kwa wananchi.



























