Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Kikundi cha Wanashinyanga tusaidiane kimezinduliwa rasmi, ambacho kimekuwa na manufaa makubwa, kwa kusaidia pale watu wanapopatwa na misiba.
TAZAMA VIDEO UZINDUZI WA KIKUNDI👇👇
Kikundi hicho kimezinduliwa rasmi leo Oktoba 14, 2026 na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo.
Akisoma Risala Katibu na kikundi hicho Kristina Kesi, amesema kilianzishwa rasmi Machi 12,2026 kikiwa na wanachama 380 na hadi leo kinapozinduliwa kina jumla ya wanachama 792.
Amesema, lengo la kuanzishwa wa kikundi hicho ni kusaidiana wakati wa msiba, kuimarisha undugu, mshikamano miongoni mwa wanashinyanga, kujenga utamaduni na kupendana, sababu mtu ni watu.
“Michango yetu ambayo tunatoa kwenye misiba kwa mtu akifiwa na mume, mke, mtoto, wazazi, mlezi, atapewa sh. milioni tatu, akifa mwanachama mwenyewe sh. milioni tano, tengemezi moja sh. milioni 1.5,” amesema Kesi.
Aidha, amesema kupitia umoja huo yamepatikana mafanikio mengi ambapo hadi sasa wameshatoa huduma ya michango kwa wafiwe yenye jumla ya thamani ya sh. milioni 80.
Amesema mbali na mafanikio hayo lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya wanachama kuchelewa kurudisha marejesho, kutoingia mara kwa mara kwenye magroup, baadhi ya wanachama kudanganya misiba, wengine kutoendelea kutoa michango baada ya wao kupewa huduma walipopatwa na msiba.
Ametaja mipango endelevu kuwa ni kuendelea kutoa huduma kwa wanaumoja kwa wakati na kwa umakini, kusajili umoja wao kisheria, kufuatilia wanachama kwa ukaribu ili waendelea kuwa wanachama hai, pamoja na kuwafuatilia na kuwachukulia hatua watakao acha umoja mara baada ya kupata huduma.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo, amepongeza kuanzishwa kwa umoja huo wa kusaidiana, kwamba kwa sasa hali ya maisha yamekuwa na gharama kubwa ikiwamo kufanya maziko.
Aidha, amelaani kitendo cha baadhi ya wanachama kudanganya misiba kwa lengo la kujipatie pesa kwa utapeli wa kishamba, na kuwataka waache vitendo hivyo siyo vya kiungwana.
Amekitaka pia kikundi hicho kuindelea kupendana, kuimarisha undugu, pamoja na kuweka mikakati ya mbeleni ili waweze kufika mbali.
TAZAMA PICHA 👇👇
Meya wa Manispaa ya Shinyaga Salum Kitumbo akizungumza.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanashinyanga Tusaidiane Yusph Mbundi akizungumza.
Katibu wa Kikundi cha Wanashinyanga Tusaidiane Kristin Kesi akisoma risala.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akikata keki kuzindua rasmi kikundi hicho.