Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, amefanya ziara katika vijiji ambavyo viliwahi kukumbwa na mafuriko miaka ya nyuma, na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kuchukua tahadhari mapema dhidi ya mvua za El-Nino, zinazotarajiwa kuanza kunyesha hivi karibuni.
TAZAMA VIDEO HAPA👇👇
Amefanya ziara hiyo leo Oktoba 7, 2026, kwa kutembelea Kitongoji cha Shilabela Kijiji cha Mwanhalanga Kata ya Samuye, pamoja na Kijiji cha Ikonda Kata ya Masengwa, maeneo ambayo yaliwahi kukumbwa na mafuriko, na pia ametembelea maeneo hatarishi, likiwamo daraja la mto manonga linalounganisha Shinyanga na Igunga.
Mhita amesema, wananchi hao wanaishi katika mkondo wa maji wa mto manonga, na wapo kwenye maeneo hatarishi ya bonde, hivyo mvua hizo za El-Nino zikianza kunyesha, watakuwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na mafuriko.
“Mvua zikianza kunyesha, msisubiri mvua izidi, bali nendeni kwenye maeneo ambayo yametengwa na halmashauri kwa ajili ya kujihifadhi, serikali haitaki kuona watu wakipatwa na majeraha kwa kuangukiwa na nyumba zao au kupoteza maisha, funga nyumba yako nenda maeneo salama,” amesema Mhita.
Amewataka pia wananchi hao, kujenga nyumba zao katika maeneo salama, na siyo kujenga kwenye maeneo hatarishi yenye mikondo ya maji.
Aidha, amewaasa pia kuhifadhi vyakula vyao, ili wasipate changamoto wakati wa mvua hizo za El-Nino.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dk. Kalekwa Kasanga, awali akitoa taarifa, amesema kijiji hicho cha Mwanhalanga kina vitongoji viwili vilivyo katika mkondo wa maji mto manonga, na kwamba mwaka 2024 kitongoji hicho kiliathirika na mafuriko, na wananchi walipelekwa kuishi kwa muda shuleni.
Aidha, amesema endapo mvua za El-Nino zikianza kunyesha, halmashauri hiyo imeshatenga eneo la wananchi hao kujihifadhi katika Shule ya Msingi Kabale.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Shilabela.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Shilabela.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ikonda.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.