` NANCY FOUNDATION YAWEKA MKAKATI WA KUWAKOMBOA WATOTO WA MITAANI SHINYANGA

WANDAMAN HOTEL

NANCY FOUNDATION YAWEKA MKAKATI WA KUWAKOMBOA WATOTO WA MITAANI SHINYANGA

 


NANCY FOUNDATION YAWEKA MKAKATI WA KUWAKOMBOA WATOTO WA MITAANI SHINYANGA

Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA

Taasisi ya Nancy Foundation, kwa kushirikiana na Ofisi ya Ustawi wa Jamii, imekutana na wadau mbalimbali wa ulinzi na ustawi wa watoto, wakiwemo watumishi wa Dawati la Jinsia, watendaji wa kata na mitaa, kwa lengo la kuweka mikakati ya kuwakomboa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani ndani ya Manispaa ya Shinyanga.

TAZAMA VIDEO👇👇


Kikao hicho, kilichofanyika leo, Oktoba 1, 2026, kililenga kuwasilisha mpango kazi wa Nancy Foundation wa kuwasaidia watoto hao na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi zinazohusika na ustawi na ulinzi wa watoto.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Nancy Foundation, Ezra Manjerenga, amesema taasisi hiyo imejipanga kupigania ustawi na haki za watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, huku utekelezaji wa mpango huo ukiwa umeanza katika baadhi ya kata za Wilaya ya Shinyanga.
Amesema Nancy Foundation inalenga kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha watoto wanaishi katika mazingira salama na wanapata malezi bora, elimu pamoja na huduma nyingine muhimu.

Sambamba na hilo, Manjerenga amezitaka taasisi za umma na binafsi kuendelea kushirikiana na Nancy Foundation katika utekelezaji wa mpango huo, ili kuwakomboa watoto wa mitaani na kuwaepusha na hatari mbalimbali wanazokabiliana nazo.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Shinyanga, Dkt. Elisha Robert, amesema Manispaa hiyo, kupitia Dawati la Jinsia, iko tayari kushirikiana kikamilifu na Nancy Foundation katika masuala ya ustawi na ulinzi wa watoto wa mitaani.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga, Lidya Kwesigabo, ameshauri kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya serikali na wadau katika kukabiliana na changamoto ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani. Amesema familia zenye uwezo zinaweza kupewa nafasi ya kuwalea baadhi ya watoto hao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Shinyanga, Penuela Samwel, ameshauri kuwepo kwa sheria na miongozo elekezi kwa taasisi na wadau wanaolenga kuwasaidia watoto wa mitaani kupitia misaada ya fedha na mahitaji mbalimbali.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuwaondoa watoto hao katika mazingira hatarishi, yakiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Aidha, Samwel amesema malezi duni na migogoro ndani ya familia ni miongoni mwa sababu zinazochangia ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika maeneo mbalimbali.

Amewataka wananchi kushirikiana na Dawati la Ustawi wa Jamii kwa kutoa taarifa kuhusu matukio na viashiria vya ukatili wa kijinsia pamoja na changamoto nyingine zinazowakabili watoto.
Nao baadhi ya watendaji wa kata na wenyeviti wa mitaa waliohudhuria kikao hicho wameipongeza Nancy Foundation kwa kuanzisha mpango huo, wakisema ni hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Wamesema serikali itaendelea kushirikiana na Nancy Foundation pamoja na wadau wengine kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi, huku watoto wakipata ulinzi, malezi na huduma stahiki.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkurugenzi wa Nancy Foundation, Ezra Manjerenga akizungumza
Afista Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga Lidya Kwesigabo akizungumza.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464